Imefahamika kuwa Rais wa Heshima na Mwekezaji Mwenza wa Klabu ya Simba SC Mohamed Dewji ‘Mo’ ndiye aliyefanikisha kuvunjwa kwa mkataba wa Kiungo kutoka Burkina Faso Ismael Sawadogo.

Simba SC ilitangaza kuachana na Kiungo huyo juzi Jumamosi (Julai Mosi) ikiwa ni muendelezo wa zoezi la kuwatema baadhi ya wachezaji ambao hawatakuwa sehemu ya kikosi cha klabu hiyo kwa msimu ujao 2023/24.

Kabla ya Ismael Sawadogo kutangazwa kuachwa klabuni hapo, alidaiwa kushinikiza kulipwa Shilingi Milioni 700 kama fidia ya kuvunjwa kwa mkataba wake, huku akikataa kutolewa kwa mkopo.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba SC zinasema, Wajumbe wa Bodi ya wakurugenzi walipata ugumu wa kumtangaza Sawadogo kutokana na shinikizo la kudai kiasi hicho kikubwa cha fedha.

“Kama sio Mo Dewji, huenda Sawadogo angeendelea kusaliwa kikosini, kwani hata jina lake si umeliona kwenye orodha ya wageni waliotakiwa kupimwa afya kesho Jumanne (Julai 04), jamaa alimpigia na kuzungumza naye na kumuahidi kumlipa fedha anazotaka akianza na nusu kwanza,” kimesema chanzo hicho cha ndani ya Simba SC na kuongeza;

“Baada ya uhakika huo wa mchezaji huyo kuridhia kulipwa kwa mafungu fedha zake, ndipo ikatolewa Thank You’ ambayo iliandaliwa tangu kitambo sambamba wenzake nane waliotemwa awali.”

Hata hivyo alipotafutwa kiungo huyo kutoka Burkina Faso na kukiri ni kweli alipigiwa simu na Dewji na kuzungumza naye juu ya kumlipa nusu ya fedha kama kianzio, kisha atamaliziwa nyingine baadae na hakuona tatizo kuendelea kukomalia msimamo wake wa awali.

“Ni kweli nilipigiwa simu na Mohammed Dewji nakuzungumza na kuafikiana naye, ameahidi kuniingiza nusu ya fedha za thamani ya kuvunjiwa mkataba wangu, nimefanya hivyo kwa heshima yake na ni mtu niliyemuelewa sana kwenye mazungumzo yetu,” amesema Sawadogo

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27 na urefu wa Mita 1.91 alisajiliwa Simba SC kwenye dirisha dogo na kucheza mechi chache kabla ya kuwa majeruhi na kuondoka kabisa kwenye kikosi cha kwanza akishindwa kuwachomoa Mzamiru Yasin na Sadio Kanoute.

Kabla ya kutua Simba SC aliwahi kung’ara na klabu za RC Kadiogo, Al Mabarra, Salitas, US Ouadadougou, Al Arabi, AS Dounes, ENPPI, Difaa El Jadida aliyoichezea jadi Januari 14 mwaka huu aliposajiliwa Msimbazi.

LATRA yaishusha ratiba ya mabasi New Force
Kocha Gamondi aanza kazi Young Africans