Mustakabali wa Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Mayele kuendelea kuwatumikia Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans msimu ujao, bado upo njia panda kufuatia taarifa za baadhi ya timu kubwa kutoka ndani ya Afrika na Bara la Asia kutaka kumsajili.

Mayele amebakiwa na mkataba wa mwaka mmoja wa kuitumikia Young Africans, lakini presha ya kumbakiza mchezaji huyo ni kubwa kwa viongozi wa timu hiyo kutokana na kiwango alichokionesha kwenye msimu uliopita katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika ambako alimaliza mfungaji bora.

Meneja anayemsimamia mchezaji huyo, Jasmine Razak amekiri mteja wake bado ana mkataba wa mwaka mmoja na klabu ya Young Africans na timu hiyo ndiyo yenye maamuzi ya kumuuza mchezaji huyo endapo itahitaji kufanya hivyo.

“Ukweli usiopingika kwamba Mayele ni mchezaji halali wa Young Africans na wao ndio wenye nafasi nzuri ya kufanya maamuzi ingawa ni kweli tunazo ofa nyingi na bado zinaingia kutoka ndani na nje ya Afrika lakini tunaheshimu mkataba na tunawapa nafasi kubwa Young Africans sababu ndio wanayemmiliki,” amesema Jasmine

Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Young Africans zinaeleza kuwa uongozi wa mabingwa hao wa soka nchini wamempa Mayele ofa ya mshahara wa Dola 12,000 ambazo ni zaidi ya Sh milioni 28 za Tanzania kwa mwezi ili asaini mkataba mpya wa miaka miwili ofa ambayo upande wa Mayele uliikataa.

Upande wa Mayele wao walitaka ofa ya mshahara wa dola 15,000 ambao ni zaidi ya Sh milioni 35 za Tanzania kwa mwezi ili asaini mkataba wa mwaka mmoja jambo ambalo uongozi wa timu hiyo ulishindwa kutoa majibu ya hapo hapo.

Inaelezwa uongozi wa Young Africans bado upo katika majadiliano kuona kama wanaweza kumudu kumpa kiasi hicho cha fedha mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu na michuano ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita.

Lakini zipo taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vikieleza kuwa Mayele ataachana na Young Africans hivi karibuni na kujiunga na timu nyingine kutoka Bara la Asia, kinachosubiriwa kwa sasa ni Mshambuliaji huyo kutumika katika utambulisho wa jezi mpya za msimu ujao 2023/24.

Sunderland: Jezi za Simba SC zipo tayari
Adha maisha ndoa yawapa msukumo kuyafikia mafanikio