Baada ya kuvutiwa na mafanikio waliyoyapata katika msimu wao wa kwanza kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara tangu ilipopanda kwa mara ya kwanza, uongozi wa Klabu ya Singida Fountain Gate, umesema upo katika mazungumzo na benchi lao la ufundi linaloongozwa na Kocha Hans van der Pluijm, ili kuendelea kukiokoa kikosi hicho.

Singida Fountain Gate, ambayo ilipanda Ligi Kuu msimu uliopita, imemaliza nafasi ya nne kwenye ligi hiyo na kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa, Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa msimu ujao 2023/24.

Benchi hilo ambalo limeiongoza timu hiyo kufikia malengo ambayo waliwekewa kabla kuanza kwa msimu wa Ligi Kuu iliyomalizika, mkataba wa Van Pluijm unamalizika hivyo, klabu hiyo ipo kwenye mazungumzo ili kocha huyo raia wa Uholanzi aendelee kuinoa na wasaidizi wake.

Msemaji wa timu hiyo, Hussein Masanza, amesema benchi lao la ufundi limekuwa na msimu mzuri na limefanya kazi yake vizuri hivyo bado wanaimani nalo.

“Benchi letu la ufundi limetimiza malengo yetu kwa asilimia 100, tumemaliza nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ambayo yalikuwa malengo ya msimu uliomalizika, limetuvusha kushiriki michuano ya kimataifa.

“Hayo ni malengo makuu mawili limetimiza na ziada kwa ni kutufikisha fainali ya Kombe la Mapinduzi na nusu fainali Kombe la Shirikisho la Soka nchini (FA Cup), kwa hiyo umekuwa msimu mzuri sana kwa kocha na benchi zima la ufundi,” amesema.

Masanza ameongeza kuwa Singida Fountain Gate FC bado ina mpango wa kuendelea na kocha huyo pamoja na benchi lake lote la ufundi.

“Mpaka sasa hakuna mabadiliko yoyote ambayo tumefanya katika benchi letu la ufundi na tunatarajia timu itaingia kambini Julai 6, mwaka huu ikiwa chini ya kocha Hans na benchi lake lote la ufundi,” amesema.

Aidha, Masanza amesema kuwa awali timu hiyo ilikuwa londoke moja kwa moja kuelekea Tunisia, lakini baada ya kikao cha

bodi ya wakurugenzi ambacho kilikaa kwa mara ya kwanza wiki  iliyopita, kimefikia makubaliano kwamba wachezaji wote ambao wamekwenda likizo na wale ambao wamesajiliwa wakutane kwanza ili wafahamiane wafanye mazoezi kwa pamoja kabla ya kuelekea Tunisia kwenye kambi ya majuma mawili.

Diaspora waombwa kuchangamkia fursa za uwekezaji NSSF
Kamati ya Ruto, Raila kujadili mambo muhimu Kitaifa