Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Makatibu Tawala wa Wilaya zote Tanzania Bara kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia utawala bora, miiko na maadili ya viongozi wa umma.
Majaliwa ametoa maagizo hayo hii leo Julai 04, 2023 wakati akifungua semina elekezi kwa Makatibu Tawala wa Wilaya katika ukumbi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dodoma na kuwasisitiza viongozi hao kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma katika maeneo yao.
Amesema, “kila mmoja akazingatie utumishi wa umma unaongozwa kwa misingi ya sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya Serikali. Misingi hiyo, ndio chachu ya ujenzi wa taswira nzuri ya Serikali ya Awamu ya Sita.”
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema lengo ya mafunzo hayo ni kuwaongezea weledi viongozi hao ili kuimarisha utawala bora.
Mafunzo hayo ya siku tatu yameandaliwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Taasisi ya Ungozi yamehusisha Makatibu Tawala wa Wilaya 135 za Tanzania Bara.