Steven Gerrard limekuwa jina jingine kubwa la hivi karibuni zaidi kuhamia kwenye soka la Ligi Kuu ya Saudi Arabia, Saudi Pro League, baada ya kuteuliwa kuwa meneja mpya wa Al Ettifaq.
ESPN iliripoti kwamba kocha huyo mwenye umri wa miaka 43, alianza tena mazungumzo na klabu hiyo baada ya awali kukataa ofa ya kujiunga nao mwezi uliopita.
Nahodha huyo wa zamani wa Liverpool, ambaye alitimuliwa na Aston Villa Novemba mwaka jana ikiwa ni chini ya miezi 12 akiwa pale Villa Park, sasa atachukua jukumu la kuinoa klabu hiyo yenye maskani yake Dammam.
Kwa mujibu wa ESPN, Gerrard alikuwa tayari kuhamia Saudi Arabia baada ya majadiliano zaidi na uongozi wa klabu.
“Mahali ambapo magwiji wanapatikana. Tunafuraha kumtangaza Steven Gerrard ndiye kocha wetu mpya,” ilisomeka taarifa ya Al-Ettifaq ikiandikwa kwenye ukurasa wake wa Twitter.
“Yeye si mgeni. Ni gwiji ambaye analeta historia tukufu na mustakabali wa kusisimua kwa Ettifaq.” iliongeza taarifa hiyo.
Rais wa Klabu, Khalid Al-Dabal, alionesha furaha yake baada ya Gerrard kusaini mkataba wa miaka miwili.
Al-Dabal alielezea mpango huo kama moja ya maarufu na ushawishi mkubwa katika Ligi ya Saudi Pro League.
Al Ettifaq ilikuwa haina kocha wa kudumu tangu kocha Mfaransa Patrice Carteron alipoondoka katika klabu hiyo Februari mwaka huu.
Lakini wamemteua Gerrard kama chaguo lao la kuijenga upya timu hiyo baada ya kumaliza nafasi ya saba kwenye Ligi Kuu yenye timu 16 msimu uliopita alama 35 nyuma ya mabingwa Al Ittihad, ambao wamemuongeza fowadi wa Real Madrid, Karim Benzema kwenye kikosi chao.
Gerrard, ambaye aliiongoza Rangers kutwaa taji lao la kwanza la Scotland ndani ya miaka 10 mwaka 2021, alikuwa pia anahusishwa na nafasi za ukocha katika Klabu za Leicester City na Leeds United zote zilishuka daraja kutoka Ligi Kuu msimu uliopita.
Nahodha huyo wa zamani wa Timu ya Taifa ya England anajiunga na kundi la watu mashuhuri waliotimkia Saudi Arabia hivi karibuni, wakiwamo Benzema, Cristiano Ronaldo na N’Golo Kante.