Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans umerudi tena kwa kocha wao msaidizi, Mrundi, Cedric Kaze na kumpa ofa mbili, kati ya hizo achague moja itakayomrejesha na kumpa mkataba mwingine wa kuendelea na majuku yake.
Awali Young Africans ilimpa ofa kocha huyo ambaye alizikataa baada ya kikao alichokaa na viongozi wa timu hiyo, kabla ya kwenda mapumzikoni Dubai.
Mrundi huyo ambaye amemaliza mkataba wake kikosini hapo, alitoa sharti la kuboreshewa maslahi yake ili asaini mkataba mpya, huku aking’angania apewe nafasi ya ukocha mkuu sambamba na kuongezewa mshahara mara mbili ya ule aliokuwa akilipwa mwanzoni.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo zimepatakana kutoka klabuni hapo, bado mazungumzo yanaendelea kati ya uongozi na kocha huyo, ndani ya juma hili itajulikana hatma yake.
Mtoa taarifa huyo amesema uongozi huo umempa ofa mbili kocha huyo kati ya hizo achague moja ambazo ni kuwa kocha msaidizi au Mkurugenzi wa Ufundi.
“Juma hili itajulikana hatma ya Kaze, kama ataendelea kufanya kazi na kocha mpya Gamondi (Miguel) ama hatoendelea kufanya kazi ndani ya Young Africans.
“Kikubwa uongozi unataka kumalizana naye ili mara timu itakapoingia kambini kuanza Pre Seasson Jumatatu ijayo awepo sehemu ya timu,” amesema mtoa taarifa huyo.
Afisa Habari wa Young Africans, Ally Kamwe, hivi karibuni alizungumzia hilo la Kaze na kusema: “Hatma ya Kaze ndani ya Young Africans ipo kwa kocha wetu mpya, kumbakisha au kumuondoa, hivyo tusubirie uamuzi wake.’