Mchakato wa mauzo ya Klabu ya Manchester United umeripotiwa upo kwenye hatua ya kukamilika muda wowote.

Hilo linaelezwa Sheikh Jassim bin Hamad Al Thani yupo kwenye hatua nzuri ya kushinda vita hiyo ya kuwa mmiliki mpya wa Man United kutoka kwenye mikono ya familia ya Glazer.

Familia ya Glazer walianza kuiweka Man United sokoni tangu Novemba mwaka jana. Awali waliweka muda wa mwisho wa mchakato huo kuwa Machi ili kufanya timu hiyo kuwa na muda wa mambo yake kwenye dirisha la usajili.

Hata hivyo, mchakato huo haukukamilika mapema kutokana na kuwapo na ofa nyingi. Na mwishowe, vita ilibaki kwa matajiri wawili, Sir Jim Ratcliffe na Sheikh Jassim.

Ratcliffe anataka awe mmiliki mpya wa Man United, lakini akitaka kuifanya familia ya Glazer kuendelea kuwapo kwenye bodi, wakati Sheikh Jassim mpango wake ni kuimiliki miamba hiyo ya Old Trafford kwa asilimia 100.

Sasa taarifa kutoka Qatar zinadai kwamba dili lipo hatua za mwisho kukubalika baada ya familia ya Glazer kuweka saini kwenye nakara zote muhimu. Watu wa kambi ya Sheikh Jassim wameanza kufurahia ushindi.

Mchakato huo ulitarajia kutangazwa jana, huku beki wa zamani wa Man United, Rio Ferdinand akidai kuna msuguano wa mawazo baina ya wana familia ya Glazer na ndio waliochelewesha mchakato huo.

Rio amesema: “Nina taarifa kutoka kwa chanzo changu cha kuaminika ndani ya Manchester United. Mambo yapo vizuri, yanakwenda vizuri japo kuna msukuano kidogo.

Unajua kitu kinapokuwa cha watu wengi tofauti na kinapokuwa chini ya mtu mmoja, mambo yanakuwa mengi na ugumu wakati mwingine.”

Dakika 270 kupima mastaa Simba SC 2023/24
Cedric Kaze aitwa tena mezani Young Africans