Mshambuliaji mkongwe, Elias Maguri amewekewa mkataba wa mwaka mmoja mezani na mabosi wa Geita Gold ili kuusaini kubaki katika kikosi hicho alichojiungana nacho Dirisha Dogo baaada ya ule wa awali kumalizika, huku akisema atatoa maamuzi juma lijalo.

Maguri aliyewahi kuzichezea Tanzania Prisons, Simba SC, Ruvu Shooting, KMC na Stand United amemaliza mkataba wa miezi sita aliusaini Januari mwaka huu na viongozi wa Geita wanapambana kumbakisha kutokana na kukoshwa na kiwango chake.

Mwenyekiti wa timu hiyo, Leonard Bugomola amesema wameweka mkataba wa mwaka mmoja kwa Maguri wakati wanaendelea kupambana abaki kikosini kwa kiwango alichokionyesha kwa muda mfupi tangu ajiunge nao na mkataba wake kumalizika mwezi uliopita.

“Bado tunahitaji kuendelea naye ndio maana tunapambana abaki, kwa sasa wachezaji wote wapo mapumzikoni lakini watakaporudi tu tutampa nafasi ya kuupitia ili kumsainisha kwa ajili ya msimu ujao,” amesema Bugomola.

Maguri amesema juma lijalo ndio atajua hatima yake kama atabaki Geita au ataenda kusaka changamoto sehemu nyingine na kwa sasa anaendelea na mapumziko kwanza.

Msimu uliopita Maguri alionyesha kiwango bora kwani katika Ligi Kuu Bara alifunga jumla ya mabao matano.

Geita inaboresha kikosi hicho baada ya kuachana na mastaa wanane wakiwemo Daniel Lyanga, George Wawa, Deusdedith Okoyo, Shinobu Sakai, Arakaza MacArthur, Shown Oduro, Jeremiah Thomas na Mussa Gadi.

Wanaobeza uwekezaji bandari waonywa
Usajili 2023/24 wamgwaya Harry Maguire