Gwiji wa klabu ya Borussia Dortmund, Marco Reus ametangaza kuachana na unahodha wa klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani ‘Bundesliga’.

Kiungo huyo wa kimataifa wa Ujerumani, amekuwa nahodha wa Dortmund kwa miaka mitano alipokabidhiwa kitambaa hicho 2018 na kocha Lucien Favre.

Akiwa sehemu muhimu ya kikosi tangu alipotua 2011, Reus alijikuta kwenye wakati mgumu msimu uliopita wakati alipokuwa akikosa nafasi kikosi cha kwanza cha Dortmund.

Na hilo ndilo lililomfanya afikie uamuzi huo wa unahodha wa timu hiyo, huku akitangaza hilo kupitia kwenye video yake aliyoposti Twitter. kuutema Kwenye video hiyo, Reus alisema: “Ni muhimu kwangu kuwaeleza hili mwenyewe. Nilitumia muda wangu mwingi wa kufikiria hili nilipokuwa mapumziko kwamba sasa naachana na kitambaa cha unahodha.

“Niliwaambia hili Edin Terzic na Sebastian Kehl. Kupata ruhusa ya kuvaa kitambaa hiki kwa miaka mitano ilikuwa heshima kubwa. Nawashukuru kwa sapoti yetu kwa miaka yote hiyo, nawatakia Edin na Sebastian uteuzi mwema wa mrithi wangu.”

Jambo hilo ni kama pigo jingine kwa Dortmund, ambao kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi wamempoteza kiungo wao Jude Bellingham, aliyemtimkia Real Madrid kwa ada ya Pauni 115 milioni.

Reus, mwenye umri wa miaka 34, hatarajiwi kuondoka klabuni hapo ambapo ataingia msimu wake wa 12, akiwa amefunga mabao 161 na asisti 121 katika mechi 387 alizotumikia miamba hiyo maarufu kama BVB.

Alisaini mkataba wa mwaka mmoja Aprili, hivyo ataendelea kubaki hapo hadi mwishoni mwa msimu ujao. Mats Hummels anapewa nafasi kubwa ya kuwa nahodha.

Ummy achukizwa na kitendo cha muhudumu wa afya Amana Kivule
Wanaobeza uwekezaji bandari waonywa