Naibu wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amewataka waajiri wote nchini, kuhakikisha wanawasilisha michango wa wafanyakazi wao kwa wakati katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Katambi ametoa agizo hilo wakati alipotembelea mabanda ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ikiwemo NSSF, PSSSF na WCF leo Julai 6, katika katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara ‘Sabasaba’ yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Amesema, “haikubaliki waajiri kutowasilisha michango ya wafanyakazi wao katika Mifuko na Serikali itahakikisha wasiotekeleza wanachukuliwa hatua za kisheria.”
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Dr.John Mduma akizungumza kwa niaba ya wakurugenzi wakuu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ikiwemo NSSF na PSSSF amesema kuwa Mifuko hiyo itahakikisha inaendelea kuboresha mifumo ya TEHAMA, ili kurahishisha uapatikanaji wa huduma.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Wakala uwezeshaji wananchi kiuchumi Zanzibar, Juma Burhan Mohamed amesema amefurahishwa na utaratibu waliowekewa wajasiriamali katika kuhakikisha wanajiwekea akiba zao za uzee na kaupata haki ya Hifadhi ya Jamii kama ilivyo kwa watumishi wengine wa sekta rasmi.