Waziri Afya Ummy Mwalimu amekemea kitendo kilichofanywa na muhudumu wa afya katika Hospitali ya Amana Kivule na kusema kuwa hakikubaliki na kinyume cha taratibu na sheria za afya.
Ametoa kauli hiyo baada ya kusambaa kwa kipande cha video kikimuonyesha muhudumu wa afya katika Hospitali hiyo akisafisha vifaa vya hospitali ikiwemo mikasi kwa Maji Baridi ya Bomba, vifaa vilivyotumika kuhudumia wagonjwa vikiwemo vya upasuaji kinyume na taratibu za kiafya.
Waziri Ummy amesema “Nimeona clip inayohusu Mtumishi wa Afya akichambua, kusafisha na kuanika vifaa vya Hospitali katika Hospitali ya Kivule mkoani Dar es Salaam.
“Kitendo hiki ni kinyume na taratibu na miongozo ya Kanuni za Udhibiti wa Maambukizi (Infection Prevention and Control). Tayari viongozi wa Mkoa wa Dar es salaam wanalifanyia kazi suala hili na watatoa taarifa rasmi.”Amesema
Na kuogeza kuwa, “Ninamshukuru mwananchi alierekodi na kuisambaza clip hii. Nitoe wito kwa wananchi kutoacha kuibua mambo kama haya yanayotokea katika vituo vyetu vya kutoa huduma za afya vya umma na binafsi ili kuongeza uwajibikaji katika utoaji wa huduma za afya nchini kwa kuwa afya zetu ni wajibu wetu”.
Ametao rai kwa wataalamu wa afya kuzingatia mafunzo na miiko ya kazi zao na kuacha kufanya kazi kwa mazoea
“Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais -Tamisemi tutaendelea kuchukua hatua ili kuimarisha ubora wa huduma.”Amesema waziri Ummy.