Kocha Mkuu mpya wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Miguel Gamondi amesema malengo yake ni kuhakikisha kuwa anawatengeneza wachezaji wake kuweza kucheza zaidi ya nafasi moja, lakini wote wawe wanauwezo wa kuleta ushindani utakaokuwa na msaada ndani ya timu.
Gamondi ambaye ni raia wa Argentina tayari ametua nchini tangu Ijumaa (Julai 07) kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya akiwa na Young Africans mara baada ya Nasreddine Nabi kuondoka.
Akizungumza kuelekea msimu mpya 2023/24, Kocha Gamondi alisema moja kati ya mambo ambayo anayatamani ni kuona wachezaji wake wakiwa wana uwezo wa kucheza zaidi ya nafasi moja huku pia akiwekea mkazo wa kuwa na wachezaji ambao wanaweza kutoa changamoto kwa wengine ili ushindani uwe mkubwa.
“Ili kuupata ubora ambao ni mkubwa ndani ya timu lazima tuhakikishe kuwa tunapata wachezaji ambao wataleta ushindani mkubwa kwa wachezaji wenzao na hiyo itakuwa ni chachu kubwa kwa kuleta mafanikio ndani ya timu kwa kuwa tutanufaika na ushindani wao.
“Kwa upande wa nafasi pia tunatakiwa kuwa na wachezaji ambao wanaweza kucheza nafasi zaidi ya moja ili kuwa na matumizi ya ziada pale ambapo kuna shida ama tatizo, kikubwa ni sisi kupata mafanikio na ndio maana mipango lazima iwepo,” amesema kocha huyo.
Young Africans ilitarajiwa kuanza kambi ya kujiwinda na msimu ujao jana Jumatatu (Julai 10) pale Avic Town, Kigamboni nje kidogo ya jiji la Dar.