Usajili ambao unazidi kufanywa na Simba SC umewaibu Young Africans huku wao wakiweka wazi kuwa wala hawatishiki, na badala yake wao wanajikita zaidi na usajili wao ili waweze kufikia malengo ya msimu unaotarajiwa kuanza mwezi Agosti.
Simba SC mpaka sasa tayari wameshatambulisha vifaa vya maana vya kimataifa vitatu ambavyo ni beki kutoka Cameroon, Che Fonde Malone, winga kutoka Cameroon, Willson Esomba Onana na winga kutoka Ivory Coast, Aubin Kramo.
Akizungumzia kuhusiana na jinsi Simba ambavyo wanafanya usajili kulingana na ukimya wao Young Africans, Afisa Habari wa klabu hiyo Ally Kamwe amesema kuwa wao wapo katika kujikita na maandalizi yao na wala hawawaangalii wapinzani wao wanafanya usajili wa wachezaji gani, huku akiahidi kuwa vifaa vyao vitaanza kushuka hivi karibuni.
“Young Africans sisi tunaangalia ambayo yanatuhusu, kuhusiana na mpinzani wetu sijui kasajili mchezaji gani hilo sisi halituhusu kwani kila mtu kwa sasa anafanya mambo yake na tutakutana msimu ujao kwenye ligi na michuano mingine.
“Nataka niwaambie mashabiki wetu kuwa sisi wala hatujapoa na badala yake tutaanza kushusha vyuma vya maana muda si mrefu kuanzia sasa hivyo wananchi mkae mkao wa kula kwani atakayecheka mwisho ndio atafurahi zaidi,” amesema Ally Kamwe