Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini England Ashley Young anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya baadae leo Jumanne (Julai 11), ili kukamilihsa usajili wa kujiunga na Klabu ya Everton.
Young yupo katika maandalizi ya kupimwa afya, baada ya kufikia makubaliano binafsi na Uongozi wa Everton, akimaliza mkataba wake na klabu ya Aston Villa aliyoitumikia msimu wa 2022/23.
Kabla ya kufanya maamuzi ya kukubali kujiunga na Everton, Young alikuwa anahusishwa na mpango wa kutimkia Saudi Arabia, lakini amefanya maamuzi ya kusitisha mpango huo, ili kuendelea kucheza soka nchini kwao England.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 38, anaondoka Aston Villa huku akiwa na Rekodi ya kutwaa Ubingwa wa England ‘Premier League’ na Kombe la FA akiwa na Manchester United, pia amewahi kutwaa ubingwa wa Italia ‘Serie A’ akiwa na Inter Milan.
Mbali na kucheza kama kiungo, pia Young ana uwezo wa kucheza kama Beki wa pembni, na kwa asilimia kubwa ya meneja wa Everton Sean Dyche ana mpango wa kumtumia katika nafasi hiyo.
Meneja huyo wa zamani klabu ya Burnley, ameanza mikakati ya kukiboresha kikosi cha Everton katika kipindi hiki, baada ya kukabidhiwa jukumu hilo mwezi Januari akichukuwa nafasi ya Frank Lampard aliyetimuliwa klabuni hapo.