Gwiji wa Klabu ya Manchester United, Rio Ferdinand anaamini kwamba Andre Onana ni mtu sahihi kuziba nafasi ya David de Gea, lakini amewatahadharisha mashabiki wa klabu hiyo kutarajia makosa.

De Gea aliyeitumikia miamba hiyo ya Jiji la Manchester kwa muda mrefu, ameondoka Old Trafford baada ya kukaa klabuni hapo kwa miaka 12.

Licha ya kutwaa tuzo ya kipa bora wa msimu uliopita katika Ligi Kuu England, Erik ten Hag anadaiwa kupoteza imani na kipa huyo wa Hispania kutokana na uwezo wake mdogo wa kucheza mpira kwa miguu.

Kocha huyo raia wa Uholanzi anapenda makipa wake kuwa na uwezo mkubwa wa kucheza kwa miguu wakianza mashambulizi nyuma, huku akikosa imani na De Gea kama anaweza kuwa msaada katika hilo.

Hata hivyo, Ten Hag anaamini kuwa amepata mtu sahihi wa kucheza katika aneo hilo baada ya kupendekeza kusajiliwa kwa Onana.

Mchezaji huyo wa Inter Milan anatajwa kuwa kipa wa kisasa, ambaye anaonekana kuwa ni aina ya mtu anayetakiwa na kutosha katika aina ya uchezaji wa Ten Hag, akiwa amefanya naye kazi akiwa Ajax.

Onana anasifika kwa kuwa na utulivu anaporudishiwa mpira na kucheza katika maeneo yote ya 18, kitu kinachopendwa na Ten Hag.

“Kama Onana atasajiliwa, naamini ni kipa mzuri na utakuwa usajili bora,” Ferdinand aliiambia chaneli ya FIVE ya YouTube. Ni mchezaji mwenye kipaji na kipa wa kisasa.

“Anaporudishiwa unamuona ana utulivu hata akiwa anafuatwa na mshambuliaji. Anaanzisha mashambulizi, anawaita wenzake na anajiamini kuomba pasi, mabeki hawana wasiwasi juu yake.

“Naamini kutakuwa na makosa tu, kutokana na jinsi pia anavyocheza, unapocheza kwa miguu kwa kujiamini namna ile, mara zote makosa hayakosekani.

“Lakini unatakiwa kubaki katika imani yako, jinsi ya kutafuta uwiano kikosini na kujua kuwa unatafuta mtu sahihi katika eneo sahihi.

“Ni vizuri kuona jinsi timu inavyoandaliwa, lakini hili ni suala ambalo kila shabiki anatamani kuona linatokea wakati huu wa usajili.”

Man United ilituma ofa nyingine jana Jumatatu (Julai 10) kwa ajili ya kumsajili Onana inayofikia Pauni 43 milioni, ikibaki kuwa klabu pekee katika mbio za kumsajili nyota huyo wa kimataifa wa Cameroon.

Kupitia Inter Milan inaaminika kwamba miamba hiyo inahitaji dau linalokaribia Pauni 50 milioni, kama itakuwa katika nafasi nzuri ya kumwachia kipa huyo kuondoka.

Che Malone: Nimekuja kufanya kazi Simba SC
Ihefu FC kumng'oa Pascal Wawa