Wachezaji sita wa Mabingwa wa Soka Ufaransa Paris Saint-Germain wamepeleka malalamiko kwa Rais wa klabu hiyo, Nasser Al-Khelaifi kutokana na maelezo yaliyotolewa na Mshambulaiji wa miamba hiyo, Kylian Mbappe.

Mfaransa huyo, ambaye amekuwa kwenye sakata la usajili na klabu yake ya PSG, alisema mabingwa hao wa Ligue 1 ni timu iliyogawanyika na watu wake wanavutiwa na mambo ya umbea.

Na sasa wachezaji kadhaa, wakiwamo wapya wamechukulia jambo hilo la maneno ya Mbappe kwa umakini kubwa na kulifikisha kwa mabosi wakubwa wa klabu.

Mbappe, ambaye amekuwa kwenye kikosi cha PSG tangu 2017, alidai pia klabu hiyo imefika kikomo.

Maneno yake, ambayo yamewekwa hadharani kupitia L’Equipe, yalifichua pia mchezaji huyo akisema kuichezea PSG si kitu kinachoongeza kitu katika ubora wake.

Mbappe ameshindwa kuisaidia PSG kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, taji ambalo timu hiyo inalihitaji kuliko maelezo.

Pia, Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa alidai kufeli mara kwa mara kwa timu hiyo kwenye michuano ya Ulaya ni swali ambalo linahitaji majibu ya kina kutoka kwa mabosi wa klabu hiyo ya Parc des Princes.

Mbappe ameamua asisaini mkataba zaidi wa kubaki hapo, hivyo msimu wa 2023-24 utakapofika mwisho, atakuwa mchezaji huru kuachana na miamba hiyo ya Paris.

Real Madrid inaonekana kama ni mahali atakakokwenda, lakini mabosi wa PSG hawapo tayari kumruhusu Mbappe mwenye umri wa miaka 24, aondoke bure hivyo wanaweza kumpiga bei wakati wowote.

Rais wa PSG, Al-Khelaifi alisema: “Tunataka abaki, lakini hawezi kuondoka bure. Kulikuwa na makubaliano ya mdomo na ameyaeleza wazi. Binafsi nilishtushwa na uamuzi wa kutaka kuondoka bure. Inahuzunisha kwa sababu Mbappe ni kijana shupavu.

Akiondoka bure ataiathiri klabu siyo yeye. Niliposikia hizi taarifa, nilishtuka sana.”

PSG imekuwa ikijimaarisha baada ya kumuongeza Marco Asensio na Milan Skriniar kwenye kikosi chao huku ikiwapata mastaa hao bure kabisa.

Pia, PSG imeripotiwa kumchukua kiungo wa kimataifa Uruguay, Manuel Ugarte kutoka Sporting Lisbo ikidaiwa kutoa Pauni 60 milioni.

FIFA yazifungia Kitayosce, Fountain Gate
Jap Stam: Mikel Arteta ana mtihani mzito