Kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, uongozi wa klabu ya Mtibwa Sugar umesema utafanya usajili wa nguvu utakaowarejesha kwenye ushindani kama ilivyokuwa zamani.

Ofisa Habari wa timu hiyo, Thobias Kifaru amesema kuwa watafanya usajili wa maana na suala la fedha halijawahi kuwa tatizo kwao kwani timu yao inamilikiwa na kampuni.

“Suala la pesa za usajili halijawahi kuwa tatizo Mtibwa Sugar, tunaweza kumsajili na kumlipa mshahara mkubwa mchezaji yeyote ndani ya nchi hii, sababu hii ni kampuni inayojiweza na tutalithibitisha hilo kwenye dirisha hili la usajili,” amesema.

Amesema mpaka sasa tayari wamekamilisha usajili wa wachezaji watano, wote wazawa na wamepanga kuwatambulisha mara baada ya taratibu zote za usajili kukamilika.

Amesema katika kikosi chao cha msimu ujao hawatakuwa na mchezaji kutoka nje ya nchi na wanafanya hivyo kwa lengo la kuinua vipaji vya wachezaji wazawa.

Kuhusiana na kocha, Kifaru amesema tayari walishapata kocha mpya atakayeifundisha timu yao msimu ujao na wanatarajia kumtambulisha hivi karibuni.

Inaelezwa kuwa kocha huyo ni Mwinyi Zahera ambaye amewahi kuifundisha Young Africans na msimu uliopita aliifundisha Polisi Tanzania ambayo ilishuka daraja.

Kilimo cha Mirungi: Viongozi Halmashauri waonywa
Hans Pluijm: Maandalizi ya kuivaa Simba yameanza