Baada ya taarifa ya kufungiwa kusajili, uongozi wa klabu ya Tabora United (Kiyatosce FC), umeliandikia barua Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ kuomba kupewa muda wa kumlipa aliyekuwa kocha wao, Ahmed El Faramawy Yousef Mostafa Soliman.

Uongozi huo umeandika barua hiyo kupitia Shirikisho la soka nchini Tanzania ‘TFF’, wakiomba pia kuruhusiwa kufanya usajili.

Tabora United imefungiwa na FIFA kufanya usajili baada ya Soliman kushinda kesi yake ya madai aliyoifungua kuwashtaki Tabora United kwa kumvunjia mkataba kinyume na sheria wakati huo ikiitwa Kiyatosce.

Mratibu wa timu hiyo, Rashid Hassan, amesema wamepokea taarifa hizo za kufungiwa na tayari wameanza juhudi za kulipa.

“Ni kweli Soliman aliwahi kuifundisha Kitayosce kwa sasa tunapambana kuhakikisha tunamlipa fedha zake, lakini tumeomba kwa mamlaka husika kutupa muda wa kulipa lakini waturuhusu kusajili,” amesema Hassan.

Kwa mujibu wa taarifa ya Afisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo amesema klabu ya Kitayosce FC na Fountain Gate, inayoshiriki Ligi ya Championship zote zimefungiwa kusajili wachezaji.

Amesema uamuzi huo umefanywa na FIFA baada ya kocha Soliman raia wa Misri kushinda kesi za madai dhidi ya klabu hizo.

“Baada ya Soliman kushinda kesi klabu hizo zitakuwa zimemlipa ndani ya siku 45 tangu uamuzi huo ulipotolewa, lakini hazikutekeleza hukumu hizo.

Wakati FIFA imezifungia klabu hizo kufanya uhamisho wa wachezaji wa kimataifa, TFF limezifungia kufanya uhamisho wa ndani,” amesema Ndimbo kwenye taarifa hiyo.

Aidha, Ndimbo kwenye taarifa hiyo amesema klabu TFF inazikumbusha kuheshimu mikataba ambayo zinaingia na wachezaji pamoja na makocha ili kuepuka adhabu mbalimbali ikiwemo kufungiwa usajili iwapo klabu inahitaji kuvunja mkataba na mchezaji au kocha inatakuwa kuzingatia sheria za mkataba.

Folarin Balogun kuipa ahuweni Arsenal
Safari ya Tanzania Kombe la Dunia 2026