Kocha Mkuu Mpya wa KMC FC, Abdulhamid Moalin, amesema kazi kubwa aliyonayo ni kukisuka upya kikosi cha klabu hiyo ili kuanza msimu mpya kikiwa imara na chenye ushindani.

Moalin alitangazwa kuwa Kocha Mpya wa KMC FC juzi Jumatano (Julai 12) akichukua mikoba iliyoachwa na Jamhuri Kihwelo Julio’ ambaye alikinusuru kikosi hicho na janga la kushuka daraja.

Akizungumza jijini Dar es salaam Moalin amesema anashukuru kupata nafasi nyingine ya kufundisha soka nchini Tanzania kwa kuonyesha uwezo wake na kutowaangusha mashabiki wa timu hiyo.

Moalin amesema anatarajia kufanya kazi yake kwa weledi ni kuifanya KMC FC kuwa moja ya timu zitakazowania mataji katika msimu mpya.

“Nashukuru Mungu kwa kupata nafasi nyingine tena ya kuifundisha timu ya Tanzania, huu ni mtihani mkubwa kwangu kwenda kuifanya timu yenye kikosi imara, najua ligi kwa sasa nchini ni ngumu na hata msimu ujao haitokuwa rahisi, lakini nimekuja hapa na nimekubali nikijua haya yote,” amesema kocha huyo wa zamani wa Azam FC.

Kuhusu atakavyokisuka kikosi chake, amesema anatengeneza kikosi ambacho si cha kuwa kusindikiza timu nyingine kama ilivyokuwa misimu iliyopita.

“Najua kwa sasa hiki walichokifanya viongozi wa KMC wanataka kuifanya klabu kuwa makini na mshindani wa kweli katika Ligi Kuu na soka la Tanzania, si msindikizaji tena, hivyo na mimi sasa nipo tayari kwa hili, nakwenda kutengeneza kikosi bora cha ushindani wa kweli wa ligi kwenye kuwania mataji,” Moalin amesema.

Moalin alitimuliwa Azam FC Agosti mwaka jana baada ya kuhudumu kama Kocha Mkuu kuanzia Januari akirithi mikoba ya Mzambia, George Lwandamina.

KMC ilinusurika kushuka daraja baada ya kuifunga Mbeya City katika mechi za mtoano, ambayo pia ilikutana na kipigo cha jumla cha mabao 4-1 kutoka kwa Mashujaa FC ya Kigoma ambayo ilifanikiwa kupanda daraja.

Rais FC Barcelona aipiga kijembe Real Madrid
Tafiti za kiuongozi zifanyike kimkakati - Simbachawene