Kocha Mkuu wa Manchester United, Erik ten Hag, amemmwagia sifa mchezaji wake mpya Mason Mount, huku akisisitiza ataisaidia timu kufanya vizuri katika michuano mbalimbali msimu ujao.

Manchester United, juzi Jumatano (Julai 12) iliibuka na ushindi wa bao 2-0, katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Leeds United, kujiandaa na msimu mpya uliofanyika Uwanja wa Ullevaal, Norway.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24 alionyesha kiwango bora katika mchezo huo baada ya kucheza dakika 45 za kwanza.

Mount, aliyesajiliwa na Manchester United hivi karibuni akitokea Chelsea kwa dau lililoripotiwa kufikia Pauni Milioni 55, alionyesha kiwango bora katika mchezo huo wakati wa kipindi cha kwanza kabla ya Kocha Ten Hag kubadilisha wachezaji wote 11 wakati wa kipindi cha pili.

Kocha Ten Hag amesisitiza kuwa mchezaji huyo atafanya makubwa ikiwemó kuisaidia timu kupata mataji mbalimbali kuanzia msimu ujao.

“Mount ni mmoja wa wachezaji wazuri na wenye kiwango bora ambao tumewasajili katika msimu ujao, ameonyesha kiwango bora mechi yake ya kwanza na kikosi chetu.

“Nina imani ataongeza nguvu na kutusaidia kufikia malengo ya kutwaa mataji mbalimbali katika msimu ujao.

“Mchezaji anayecheza nafasi ya kiungo, ana uwezo wa kuzuia mashambulizi na kucheza nafasi ya beki pale anapohitajika, ninaamini ataongeza nguvu zaidi katika safu ya kiungo.

“Ni mchezaji bora na mwenye kiwango cha hali ya juu, ushirikiano wake utaisaidia Manchester United kufikia malengo tuliyojiwekea katika msimu ujao,” amesema Kocha Ten Hag.

Kocha huyo alianza na kikosi cha kwanza akiwa na wachezaji vijana wenye uzoefu, baadhi yao ni Lisandro Martinez, Raphael Varane, Jadon Sancho Kobbie Mainoo na Omari Forson.

Twaha Kiduku: Dullah Mbabe atambamiza Katompa
Mashujaa FC yaanza na Mshambuliaji wa Mtibwa Sugar