Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu mkazi wa Dar es Salaam, Omari Juma kunyongwa hadi kufa baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumuua kwa kukusudia aliyekuwa mlinzi wa Kanisa la Moravian Tabata Segerea, Timoth Kyage.
Hukumu hiyo, imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Pamela Mazengo wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu, huku Mahakama hiyo ikimuachia huru Ramadhani Omari baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.
Ilielezwa kuwa, Agosti 21, 2017, Omari pamoja na wenzake watatu waliruka ukuta wa kanisa hilo na kumvamia Timoth kisha kumfunga mdomo na pua kwa plasta ili asipige kelele na kumfunga miguu na mikono kutumia kamba za katani kisha kumpiga na kumjeruhi vibaya.
Akisoma hukumu hiyo, Pamela alisema kuwa wakati wa uendeshwaji wa kesi hiyo mshtakiwa huyo alikiri kosa na kuieleza mahakama kuwa walivamia kanisa hilo baada ya kupewa taarifa na rafiki yake kuwa kulikuwa na fedha ndani ya kanisa hilo hivyo waliingia kwa ajili ya kuziiba japo hawakuzikuta.
Wakati tukio hilo likiendelea mlinzi wa kanisa la jirani ambalo ni Kanisa Katoliki aligundua kuwa kuna uvamizi unaendelea kanisani hapo kisha kupiga risasi angani jambo lililowafanya wahalifu watatu kukimbia na alibaki Omari aliyeshindwa kukimbia baada ya kudhibitiwa.
Uchunguzi wa Daktari ulionesha kuwa marehemu alipigwa na kitu kizito katika sehemu ya kichwa chake kiasi cha kupelekea ubongo kuonekana pia alikosa hewa kutokana na kuzibwa pua na mdomo hali iliyompelekea kupoteza maisha.