Uongozi wa Maafande wa Jeshi la Magereza Tanzania Prisons umesema kuwa katika dirisha hili la usajili hawatowapa kipaumbele wachezaji wanaoachwa na timu kubwa za Young Africans, Simba SC na Azam FC.
Mwishoni mwa juma lililopita Prisons ilifanikiwa kumsainisha kiungo Salum Kihimbwa na kumpa mkataba wa miaka miwili kutumikia kikosi cha timu hiyo chenye maskani yake jijini Mbeya.
Kihimbwa aliyewahi kupita kwenye timu za Mtibwa Sugar, Dodoma Jiji na Mbeya City ametua kwa maafande hao kwa ajili msimu wa 2023/24.
Mwenyekiti wa timu hiyo, Enock Mwanguku amesema mchakato wa usajili unaendelea vizuri kwa kuzingatia maelekezo kutoka kwa kocha wao mkuu Fred Minziro.
“Hatusemi kwamba hatutawachukua ila malengo yetu kuwapa nafasi vijana ila tukiwapata waliotoka katika timu hiyo basi tutaangalia ambao wanaendana na mfumo wa timu yetu,” amesema Mwanguku.
Amesema wakati wakiendelea kufanya usajili wanazingatia zaidi mipango yao kwa kuangalia vigezo vyao vya usajili kwa kuwapa nafasi kubwa wachezaji vijana zaidi kuimarisha kikosi cha timu yao.
Ameongeza kuwa kikosi cha timu hiyo tayari imeshaanza maandalizi ya msimu ujao kwa wachezaji kukutana kwenye maskani yao jijini Mbeya kabla ya Agosti Mosi, mwaka huu kuelekea Visiwani Zanzibar.