Baada ya ya kuanza maandalizi yao rasmi ya msimu mpya wa mashindano 2023/24 huko nchini Uturuki, mastaa wote wa Simba SC juzi Jumamosi kwa mara ya kwanza walifanyiwa vipimo vya uzito kwa ajili ya kutengenezewa programu mpya ya utimamu wa mwili.
Sehemu ya kikosi cha Simba SC ambao wako nchini Uturuki kujiandaa na msimu mpya ambapo walianza rasmi programu za mazoezi Julai 13, mwaka huu walipimwa uzito kwa mara ya kwanza kwa ajili ya kufanya tathimini ya utimamu wao wa mwili, ili kupangiwa vyakula ambavyo wanapaswa kutumia katika kipindi hiki cha maandalizi.
Baada ya vipimo hivyo vilivyofanyika asubuhi, jioni wachezaji walifanya mazoezi magumu ya uwanjani ambapo walitakiwa kukimbia muda mwingi, ili kujaza pumzi.
Kocha msaidizi, Ouanane Sellami alipozungumzia kuhusiana na programu hiyo alisema kwa mujibu wa programu iliyopo, wachezaji wataendelea kuwa na mazoezi magumu kwakuwa ndivyo inavyotakiwa hasa mwanzoni mwa maandalizi ya msimu.
Sellami amesema: “Mazoezi tuliyofanya katika siku hizi za awali yalikuwa na umuhimu wa kuongeza utimamu wa kila mchezaji ndio maana tuliwaweka vifaa maalumu (GPS), kwenye vifua vyao ili kuona yupi amefika pale panapohitajika na nani anatakiwa kuongezewa, au kupungiziwa ili wote kuwa sawa.
“Mwishoni mwa maandalizi haya tutapunguza ugumu wa mazoezi, ikiwemo kucheza mechi za kirafiki ili kuona tunachowapatia wachezaji kwa wakati huu wamekifanyia kazi kwa kiasi gani.”