Baada ya kuripotiwa juu ya Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kutimka kambini kwenda masomoni, kocha huyo ameibuka na kufafanua juu ya ukweli wa taarifa hiyo, akikiri atakuwa nje ya timu kwa muda wa juma moja.

Awali ilifahamika kwamba Robertinho aliondoka kambi ya timu hiyo iliyopo Uturuki kwenda kusoma, lakini amesema sio anaenda kusoma bali anaenda kuwanoa makocha kwao Brazili kwani yeye ni mkufunzi.

Kocha huyo aliyetua Msimbazi mwisho mwa msimu uliopita na kuiwezesha kumaliza nafasi ya pili huku ikiifunga Young Africans mabao 2-0, amesema amerudi Brazili kwenda kutoa darasa kwa makocha.

“Ni kweli sipo na timu nipo Brazil, lakini nina ruhusa maalumu. Nitakuwa huku kwa wiki moja ili kuwanoa makocha na sio kusoma,” amesema kocha huyo wa zamani wa Vipers na kuongeza;

“Kwa sasa timu ipo chini ya Quanane Sellami akisaidiana na kocha wa viungo naamini itakuwa sawa, kwani wachezaji wanafanya zaidi mazoezi ya viungo na nimeacha programu nyingine.”

Simba SC ipo kambi ya maandalizi ya msimu mpya ikitarajiwa pia kucheza mechi tatu kabla ya kuja kuwasha moto katika Tamasha la Simba Day itakayofanyika Agosti 6 kisha kwenda kucheza mechi za Ngao ya Jamii.

Ahukumiwa kunyongwa kwa kumuuwa mlinzi
David De Gea kurudi nyumbani Hispania