Klabu ya Simba SC inaendelea kupambania mpango wa usajili wa Mlinda Lango atakayeziba pengo la Aishi Manula, ambaye anaendelea kujiuguza baada ya kufanyiwa upasuaji utakaomuweka nje ya dimba kwa miezi kadhaa.

Simba SC imedhamiria kusajili  Mlinda Lango, na inaarifiwa Uongozi wa Klabu hiyo umeelekeza nguvu zake kwa Mlinda Lango kutoka Cameroon, Simon Omossola anayeitumikia klabu ya Saint-Éloi Lupopo ya DR Congo.

Inafahamika kuwa Simba SC imeachana na dili la Mlinda Lango kutoka Brazil Caique Luis da Santos kwa sababu mbalimbali ikiwemo kigezo cha lugha, lakini sasa iko siriazi na Omossola aliyesaini miaka miwili na FC Saint Eloi Lupopo mwishoni mwa mwaka 2022.

Habari zinasema mezani mwa viongozi wa Simba SC yamebaki majina ya Walinda Mlango wawili moja ni wa Lupopo aliyetoka AS Vita ya DR Congo, Omossola mwenye umri wa miaka 25 na lingine ni la Mbrazil mwingine aliyependekezwa na kocha Robertinho baada ya dili la Caique kukwama.

Hata hivyo, Omossola anaonekana kupigiwa chapuo na viongozi wengi wa jopo la usajili hivyo wakiafikiana huenda akawa mbadala wa Beno Kakolanya na atakayeziba pengo la Aishi Manula.

Simba SC inaamini uzoefu wa Omossola katika michuano ya Kimataifa na timu ya taifa ya Cameroon vitaisaidia kufikia malengo ya klabu hiyo, hasa kuvuka kizingiti cha Robo Fainali ambacho kinaonekana kuwa mtihani mzito kukivuka kwa Wekundu hao wa Msimbazi.

Pia Omossola anazungumza Kiingereza na Kifaransa, hivyo itakuwa rahisi kuwasiliana na mabeki ingawa dau lake linatajwa si chini ya Sh400 milioni.

Wenger: Arsenal itatwaa ubingwa 2023/24
Mchakato kuwapata walengwa TASAF umulikwe - Wananchi