Aliyekuwa Mlinda Lango wa Manchester United, David de Gea, huenda akatimkia zake nchini Saudi Arabia baada ya timu kibao zinazoshiriki katika Ligi Kuu kuonyesha nia ya kutaka kumsajili na kumpa mshahara wa zaidi ya Pauni 700,000 kwa juma.

Ofa iliyokuwa ikitajwa sana ni ile ya Al Nassr, lakini kwa sasa inaonekana kuwa ngumu kukamilika kwa sababu hadi sasa timu hiyo imefungiwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kufanya usajili wa wachezaji wapya kufuatia kushindwa kuwalipa haki zao baadhi ya wachezaji iliokuwa nao kipindi cha nyuma walipoondoka.

De Gea ambaye aliachana na Manchester United katika dirisha hili la usajili huko Ulaya baada kushindwa kuafikiana na mabosi wa timu hiyo kwenye suala la maslahi, anaonekana kuwa hataki kuendelea kucheza tena barani Ulaya kutokana na ofa nono iliyowekwa na Waarabu wa Saudi Arabia.

Mlinda Lango huyo mwenye umri wa miaka 32, raia wa Hispania kabla ya kuachana na Mashetani Weklundu msimu uliopita alicheza mechi 58 za michuano yote na kuruhusu mabao 61.

Pamoja na timu za Uarabuni, De Gea pia anatajwa kufukuziwa na timu mbalimbali zinasoshiriki Ligi Kuu ya Marekani (MLS), ambako baadhi ya nyota aliocheza nao enzi zake kule Hispania wamekimbilia huko.

Mlinda LAngo huyu amekuwa akitajwa katika rada ya timu hizo zinazopambana kujitangaza na kuitangaza ligi hiyo katika soka la kimataifa, lakini inaelezwa kwamba huenda ikawa ngumu kutua iwapo atataka kuwafuata mastaa waliotimkia Uarabuni.

Tanzania, Hungary kuimarisha uhusiano Kidiplomasia
Mecky Mexime: Natafuta watu wa kazi