Baada ya kumwajiri Mwinyi Zahera kuwa kocha mkuu wa Coastal Union, uongozi umemrejesha Fikiri Elias kuwa Kocha msaidizi.

Msimu wa Ligi Kuu Bara ulipomalizika, uongozi ulivunja benchi la ufundi na sasa umeanza kutengeneza upya huku baadhi ya waliokuwepo wakirejeshwa.

Awali Fikiri ndiye aliyekuwa kocha mkuu akisaidiwa na Joseph Lazaro. Mwingine aliyerejeshwa ni mtunza vifaa, Mathayo Francis huku ikimwajiri kocha mpya wa makipa Alawi Mansour aliyemrithi Salim Waziri.

Msemaji wa klabu hiyo, Jonathan Tito amesema bado nafasi mbili hazijajazwa ambazo ni ya daktari na meneja. Nafasi hizo awali zilikuwa chini ya Francis Mganga (daktari) na Kuha Idd (Meneja).

Kuhusu kambi ya timu, Tito amesema: “Inaanza Jumatano (kesho) ingawa kuna baadhi ya wachezaji wanaendelea na mazoezi binafsi ila rasmi ni hadi Jumatano kwani makocha watakuwa wamerejea.

“Zahera alikwenda Arusha kukamilisha mambo yake. Fikiri pia anakuja huku (Tanga). Kuhusu usajili tunaendelea nao. Tumewarudisha baadhi yao kwenye benchi kutokana na mahitaji tuliyonayo. Tunaamini watatusaidia kwa kushirikiana na kocha mkuu.”

Rais Samia amlilia Jecha, Mkapa
Spika Dkt. Tulia ashiriki Mkutano Jumuiya ya Madola