Klabu ya Arsenal inataka kufanya usajili wa Pauni 40 milioni kwa kiungo wa Ajax, Mohammed Kudus, lakini itahitaji kuuza baadhi ya wachezaji wa Mikel Arteta ili kukusanya fedha zaidi kufikia bajeti yao ya msimu huu ya Pauni 200 milioni.

The Gunners imeshaanza kuimarisha kikosi kwa ajili ya msimu ujao, wakati ikikamilisha usajili wa Declan Rice, Kai Havertz na Jurrien Timber.

Mkurugenzi wa Michezo wa Arsenal, Edu sasa amewageukia Kieran Tierney, Cedric Soares, Nicolas Pepe, Albert Lokonga, Nuno Tavares na Rob Holding, ambao watakuwa katika nafasi nzuri ya kuuzika sokoni.

Majaliwa ya Thomas Partey yatajulikana pia msimu huu, lakini inaaminika kwamba Arsenal inataka kumuuza nyota huyo wa kimataifa wa Ghana kama kutakuwa na ofa kubwa kwa ajili yake.

Lakini wakati ikiangalia kuuza wachezaji, Arsenal inataka kuongeza mchezaji mwingine katika eneo la kiungo na nyota huyo wa Ghana anaonekana kuivutia zaidi miamba hiyo ya Kaskazini mwa London.

Mchezaji huyo mwenye miaka 22 anaweza kucheza katika nafasi zote za eneo la kiungo wa kati, ambalo pia linampa nafasi ya kusogea mbele kwa ajili ya kuongeza nguvu katika ushambuliaji ama winga wa kulia.

Uwezo wake wa kucheza nafasi nyingi uwanjani unaonekana kuwa kitu muhimu ambacho kinaisukuma Arsenal kutaka kumsajili.

Kudus pia anatakiwa na Brighton, lakini matamanio yake ya kutaka kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya ndiyo yanampa nafasi kubwa kusajiliwa na Arsenal.

Wakati huo huo, Arsenal imeanza mchakato wa kuziba nafasi iliyoachwa na mtaalamu wa tiba, Gary O’Driscoll, ambaye alijiunga na Manchester United msimu huu.

O’Driscoll anatarajiwa kutoa taarifa rasmi muda wowote kabla ya kuanza majukumu yake mapya ndani ya Old Trafford, akiacha nafasi kwa klabu hiyo kutafuta mtu mwingine.

Mail Sport liliandika kuwa bosi wa wataalamu wa tiba wa Ligi Kuu England, Mark Gillett, ambaye ana uzoefu mkubwa na Ligi Kuu, awali akiitumikia Chelsea na West Brom, ni miongoni mwa wanaotarajiwa kuziba nafasi yake.

Simba SC yamsajili mbadala wa Jonas Mkude
Chama, Ngoma wana shughuli nzito Uturuki