Baada ya Mzambia, Clatous Chama na kiungo mkabaji mpya wa Simba SC, Fabrice Ngoma kujiunga na kikosi cha timu hiyo kilichoweka kambi Uturuki, uongozi wa timu hiyo umesema ari na morali ya kikosi imeongezeka zaidi.

Nyota hao waliondoka nchini jana na tayari wameshawasili Uturuki kuungana na wachezaji wenzao katika mazoezi yanayoongozwa na Kocha Mkuu, Robert Oliveira ‘Robertinho’ kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na mashindano ya kimataifa ya Super League na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema Chama na Ngoma watakuwa katika sehemu ya mazoezi yatakayofanyika leo Ijumaa na ujio wao umeongeza nguvu katika kambi hiyo.

Ahmed amesema kwa sasa wachezaji wa Simba SC wanamalizia programu ya mazoezi mepesi, na sehemu ya pili ya mazoezi magumu inatarajia kuanza juma lijalo pamoja na kucheza michezo ya kirafiki.

“Wachezaji wote watakuwapo kambini leo ljumaa  ili kuendelea na mazoezi kulingana na programu ya Robertinho, kila kitu kinakwenda vizuri na maandalizi ya mechi za kirafiki yako katika hatua za mwisho, mwalimu anataka kuona uwiano wa wachezaji wake wote.

Lini tutacheza mechi ya kirafiki, bado sijapata taarifa rasmi lakini natambua Robertinho anahitaji kupata mechi tatu kabla ya kikosi hakijarejea nyumbani, ninaimani hivi karibuni tutapata ratiba ya mechi zetu za kirafiki,” amesema Ahmed.

Ameongeza msimu ujao Simba SC haitakuwa na ‘masikhara’ kwa sababu wamefanya usajili mzuri pamoja na kutayarisha jezi ambazo zina hadhi ya kuvaliwa na timu kubwa kama Simba SC.

“Wachezaji wote ambao tumewasajili na kuwatambulisha tayari wako kambini. Ngoma na Chama, tayari wameungana na timu na kuendelea na majukumu ya kujiandaa kwa ajili ya msimu mpya, tunatarajia leo Ijumaa, kufanya utambulisho wa jezi zetu na wachezaji wetu wataonekana na uzi mpya,” amesema Ahmed.

Simba SC itatambulisha kikosi chake kipya katika siku ya Tamasha la Simba Day litakalofanyika Agosti 6, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Katika kuanza msimu mpya, Simba SC itakutana na Singida Fontain Gate katika mechi ya hatua ya Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii wakati fainali za michuano hiyo įtachezwa Agosti 13, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini, Tanga.

Wazazi nguzo kuu mapambano Dawa za kulevya
Sadio Mane kucheza Saudi Arabia