Faisary Ahmed – Kagera.

Wakulima wa zao la Vanila Mkoani Kagera, wameanza mchakato wa kuunda umoja wa AMCOS ili kukabiliana na changamoto ya kushuka kwa thamani ya zao hilo sokoni, hali inayowasababishia kudorola kiuchumi.

Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha wakulima wa hilo Manispaa ya Bukoba, Mwenyekiti wa muda wa mchakato wa kuunda Chama cha Wakulima wa Vanila, Dedani Sombe emesema wameamua kufanya hivyo kutokana na hali ya soko ilivyo na elimu ndogo waliyonayo wakulima.

Amesema, “Mkulima atanufaika kwa kupata bei nzuri ya vanila, elimu ya kukausha na ndio maana mpaka sasa hivi tumeshaanza kuunda makundi ya kujifunza kukausha na pia mkulima kupitia AMCOS atapata sauti kwa kushirikiana na serikali pia tutaweza kupata wateja kutoka nchi za nje.”

Naye Afisa ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Farida Amani amebainisha changamoto za wakulima wa zao hilo kuwa ni uhaba wa mbolea mashambani, wadudu kushambulia zao hilo na uhaba wa kupata masoko sahihi.

Amesema, “Wakulima wa vanila hawana soko la uhakika kwamba watauzia sehemu fulani ndio maana tunawashahuri wawe na uhakika watakapokuwa pamoja watakuwa na nguvu ya kusemea pamoja lakini itakuwa rahisi kwa wao kupanga bei nzuri”.

Kwa upande wake, Afisa kilimo wa Manispaa ya Bukoba, Jackson Mahongo amesema, “ni kweli bei imeporomoka kwa msimu huu tofauti na misimu iliyopita lakini ni ukweli usio pinginga kwamba serikali haipangi bei, kinachoongoza ni soko yaani wazalishaji pamoja na wanaohitaji.”

Baadhi ya wakulima wa zao la Wanila, Alex Audax na Verdiana Benedicto wameeleza kuwa mpaka sasa wapo kwenye hali ya sintofahamu kutokana kuwa bei ya zao hilo kushuka thamani na changamoto ya wizi wa Vanila mashambani ila wanaamini kuundwa kwa umoja huo itakuwa suluhisho la changamoto hizo.

Zao la Vanila mkoa wa Kagera imeshuka thamani kutoka elfu 3,0000 kwa bei ya msimu wa mwaka jana hadi kufikia elfu 15,000 na wengine kununua kwa elfu 3,000 msimu wa mwaka huu na uamuzi huo umekuja ukiwa na lengo la mkulima wa zao la vanila kumuwezeshwa kupata uhakika wa soko, ulinzi wa Vanila shambani na kupata elimu ya ukaushaji wa zao hilo.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Julai 22, 2023
Namungo, Singida FG kupasha Arusha