Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama amesema Serikali itaendelea kuunga mkono kampeni ya GGML KiliChallenge inayolenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi kwani inalandana na jitihada za Serikali kutokomeza maambukizi mapya ya ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
Pia amemwagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuhakikisha wanafunzi wawili wa miaka 14 waliopanda mlima Kilimanjaro kwa siku 7 kupitia kampeni hiyo iliyoasisiwa miaka 22 iliyopita kuingizwa kwenye orodha ya miongoni mwa watu watakaohudhuria sikukuu ya mashujaa ambayo itafanyika Julai 25 mwaka huu.
Kampeni hiyo iliyoasisiwa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini (Tacaids) mwaka 2002 pia inalenga kuisaidia serikali kutimiza malengo ya kitaifa ya kufikia sifuri tatu – kutokuwa na maambukizi mapya, kutokuwa na unyanyapaa na ubaguzi, na kutokuwa na vifo vitokanavyo na Ukimwi.
Akizungumza katika hafla ya kuwapokea washiriki 35 waliopanda mlima Kilimanjaro na 26 waliouzunguka mlima huo kwa baiskeli mwishoni mwa wiki wilayani Moshi, Mhagama alisema GGML imeonesha kitendo cha kishujaa kuratibu kampeni hiyo kwa miaka zaidi ya 22.
“Kwa hiyo GGML kujitoa kubeba maumivu ya siku saba kwa ajili ya maumivu ya watanzania, hili jambo hili ni la kijasiri, la kishujaa litaendelea kukaa kwenye vitabu vya mambo ya msingi yaliyofanywa na taasisi zetu nchini. Kwa mfano huu mzuri uliooneshwa na GGML napenda kuwaambia hongereni sana,” alisema.
Alitoa wito kwa mashirika mengine ya kitanzania na ya kimataifa kuiga mfano wa GGML kuihudumia jamii kwa moyo wa dhati na kujitoa.
Aidha, aliwapongeza washiriki pamoja na watoto hao waliopanda mlima tarehe 14 Julai mwaka huu na kushuka tarehe 20 Julai na kusisitiza kuwa ni mashujaa ambao mafanikio yao yamedhihirisha kuwa mwitikio dhidi ya VVU na Ukimwi unawezekana iwapo kutakuwa na dhamira ya dhati kwa kila Mtanzania kutokomeza janga hilo nchini.
Mmoja kati ya wanafunzi hao ambaye alifanikiwa kupanda mlima Kilimanjaro na kufika katika kilele cha uhuru ni Rebecca Damiani(14) mwanafunzi wa shule ya msingi Kivukoni na Abel Musa(14) mwanafunzi wa shule ya msingi Mbugani ambaye alirudia njiani baada ya kuugua malaria akiwa mlimani.
Wanafunzi hao ni wanatoka katika kituo cha Moyo wa Huruma – Geita ambacho kinalea watoto wanaoishi katika mazingira magumu chini ya ufadhili wa GGML.
Mhagama alisema watoto hao wameonyesha uzalendo mkubwa kwa Taifa kwa kujitosa kuungana na watanzania wengine katika kuchochea nguvu ya mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi nakwambia wanapaswa kutambuliwa kama mashujaa katika nchi.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong aliishukuru serikali kwa kuunga mkono katika mapambano hayo nakuhakikisha zinapatikana fedha kwa ajili ya kutokomeza janga la Ukimwi hapa nchini.
Aidha, aliwapongeza watoto hao kwa rekodi ya kipekee waliyoiweka na kuahidi kuwa GGML itaendelea kuwaunga mkono katika kutimiza ndoto zao.
Kaimu Mkurugenzi Tacaids, Jerome Kamwela aliwapongeza wapanda mlima hao na kusema wamekuwa mabalozi wazuri katika kuendeleza mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi hapa nchini.