Baada ya kutupia bao kwenye mchezo wa Kilele cha Wiki ya Mwananchi, Mshambuliaji Kennedy Musonda ametoa msimamo akisema ana kazi ngumu ya kufanya kwa vile anatambua kila mmoja ameweka matumaini kwake baada ya Fiston Mayele kuondoka.

Musonda alifunga hilo katika mechi hiyo ya kirafiki wa kimataifa dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ilitumika kukitambulisha kikosi kipya cha msimu ujao na baada ya mchezo huo mshambuliaji huyo Mzambia amesema nafasi aliyoipata kuitumikia timu hiyo ni kuibeba timu na amejipanga sana.

“Uongozi ndio una nafasi kubwa ya kuthibitisha kuondoka kwa Mayele, mi sifahamu ila kwa upande wangu nina mtihani mkubwa na juzi Jumamosi (Julai 22) nilikuwa nafahamu natazamwa zaidi na hili limekaa kichwani na nitapambana kuwapa raha mashabiki wa Young Africans,” amesema Musonda na kuongeza;

“Eneo la ushambuliaji ndio siri kubwa ya ushindi nimefurahi nimepata nafasi ya kufunga japo sio mabao mengi lakini hilo moja limenipa nguvu na imani kuwa inawezekana na nitatakiwa kuwa imara zaidi kwa sasabu natazamwa na wengi.”

Akizungumzia usajili kwa ujumla amesema ni mzuri na kila mchezaji aliyepata nafasi ya kuungana na Young Africans anajua nini kimemleta ndani ya timu, hivyo ni wazi watakuwa na wakati mzuri msimu ujao.

“Siwezi kumzungumzia mchezaji mmoja mmoja kubwa zaidi ni Young Africans itaendelea ilipoishia tutakuwa bora zaidi kutokana na ubora wa wachezaji walioongezeka na chachu ya namba kwa kila mchezaji.”

Mshambuliaji huyo aliyejiunga na Young Africans dirisha dogo msimu uliopita aliweka wazi atafanya kila linalowezekana kuhakikisha safu yao ya ushambuliaji inafunga mabao mengi msimu ujao.

Walitaka kumbambikia Silaha, Dawa za kulevya - Kenyatta
Mnyama kuitwa jina lako Mil. 5 - TANAPA