Timu sita za Tanzania, leo zitafahamu kama zitakutana vibonde au wapizani wagumu katika hatua za awali za michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe Shirikisho la Afrika msimu wa 2023/2024.

Droo hiyo itafanyika saa 8:00 Mchana katika Makao Makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) jijini Cairo nchini Misri, ambapo timu 52 zitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao wakati timu 51 zikishiriki Kombe la Shirikisho.

Tanzania Bara itawakilishwa na timu nne ambazo ni Young Africans na Simba SC zitakazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Azam FC na Singida Fountain Gate zitacheza Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa upande wa Zanzibar itawakilishwa KMKM na itakayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika huku JKU ikicheza Kombe la Shirikisho.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, upangaji wa Droo hiyo utaanza na timu zinazoshiriki Kombe la Shirikisho na baadae Ligi ya Mabingwa.

Young Africans imekata tiketi ya kucheza michuano hiyo baada ya kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita wakati Simba SC ikimaliza nafasi ya pili katika michuano hiyo.

Azam FC ilikata tiketi baada ya kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu pamoja na kufika Fainali ya Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ wakati Singida FG ilishika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu.

Kwa upande wa KMKM ilikata tiketi baada ya kutwaa taji la Ligi Kuu ya Zanzibar huku JKU ikiwa imetwaa Kombe la Shirikisho visiwani humo.

Klabu ya Al Ahly ya Misri ndiyo Bingwa Mtetezi wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika huku USM Alger ikiwa ndiyo Bingwa Mtetezi wa Kombe la Shirikisho.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema timu yao ipo tayari kucheza na timu yeyote watakayopangwa nayo.

“Tumejipanga vizuri kila idara, timu yeyote ambayo tutapangwa nayo tupo tayari kumenyana nayo na msimu huu tunataka tufike mbali zaidi,” amesema.

Afisa Habari wa Young Africans, Ally Kamwe amesema timu yeyote ambayo watapangiwa wapo tayari kupambana nayo, kwani safari hii wanahitaji kuwa mabingwa wa mashindano ya kimataifa.

“Tayari tuna uzoefu na mechi za kimataifa hivyo hatuogopi timu yeyote ambayo tunaenda kukutana nayo, tumejipanga vizuri tuna kikosi bora,” amesema Kamwe.

Ofisa Habari wa Singida Fountain Gate, Hussein Masanza amesema pamoja na kuwa wageni katika mashindano hayo, hawaihofii timu yeyote.

VIWANGO CAF: Katika hatua nyingine, Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limetoa orodha ya viwango vya ubora kwa klabu za Afrika baada ya kumalizika msimu wa 2022/2023.

Katika viwango hivyo, Simba SC imeshika nafasi ya tisa ikiwa na alama 35, Young Africans nafasi ya 18 kwa alama 20 huku Namungo FC ikishika nafasi ya 70 kwa alama 1.5.

Simba SC imeshika nafasi ya tisa baada ya kufanya vyema katika michuano ya kimataifa msimu wa 2022/23, 2021/2022, 2020/2021 na 2018/2019 wakati Young Africans ikifanya vyema msimu wa 2022/2023 huku Namungo FC iking’ara msimu wa 2020/2021.

Wanasiasa msipinge kila jambo la Serikali - Dkt. Kimei
Wakulima wekeni akiba, msiuze mazao yote - Dkt. Mpango