Uongozi wa Chelsea huenda ukaingia kwenye mgogoro na Mshambuliaji wake Romelu Lukaku baada ya staa huyu kuendelea kushikilia msimamo wake wa kutaka kujiunga na timu za Ulaya licha ya kwamba hadi sasa hakuna ofa zilizofika mezani.

Inaelezwa kwamba Chelsea imepokea ofa ya timu nyingi kutoka Saudi Arabia lakini Lukaku amezigomea na kusisitiza kwamba bado anataka kubaki Ulaya.

Awali, kulikuwa na tetesi kwamba fundi huyu huenda akasaini mkataba wa kudumu na Inter Milan ama akajiunga na Juventus lakini kote huko imeshindikana.

Kwa upande wa Juventus mashabiki wamekuwa wakipinga asisajiliwe kwani alishawahi kusema hatokaa aichezee timu hiyo na kule Inter, yeye mwenyewe amekataa kurudi.

Mapema katika dirisha hili kulikuwa na tetesi kwamba Al-Hilal imeweka mezani ofa ya mshahara wa Pauni 45 milioni ili kuipata huduma yake lakini alikataa.

Mshambuliaji huyo ambaye pia aliwahi kukipiga Manchester United lakini hakuwa kipenzi cha mashabiki, anaamini anaweza kufanya makubwa Ulaya hivyo muda wa kwenda Uarabuni haujawadia licha ya kwamba tayari ana umri wa miaka 30.

Lukaku ndiye mfungaji bora wa muda wote wa timu taifa ya Ubelgiji ambayo ameifungia mabao 75, akifuatiwa na Eden Hazard (33).

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Julai 26, 2023
George Mpole ajiandaa kukiwasha DR Congo