Klabu ya Simba ni kama imechulia kwa kuitaja Power Dynamos ya Zambia ambayo wameitangaza kuwa mpinzani wao katika mchezo wa kusherehesha Tamasha la Simba (Simba Day) ambalo limepngwa kufanyika Agosti 06 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Power Dynamos ambao ndio Mabingwa wa Soka nchini Zambia, pia wametajwa tena huko CAF katika hafla ya kupanga michezo ya hatua za awali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2023/24, huku ikisogezwa karibu na Simba SC ya Tanzania.

Hata hivyo wababe hao wa Zambia itawalazimu kushinda mchezo wao wa awali dhidi ya African Stars kutoka Namibia, ili kutimiza mpango wa kukutana na Simba SC katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2023/24.

Ratiba ya mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika inaonesha Mabingwa wa Soka nchini Namibia Africans Stars wataanzia nyumbani kwa kuikabili Power Dynamo, kabla ya kusafiri kuelekea nchini Zambia kwa mchezo wa mkondo wa pili.

Hata hivyo Simba SC inayomsubiri mshindi wa mchezo huo itaanzia ugenini katika mchezo wa mzunguuko wa pili hatua ya awali, kisha itamalizia nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Hatua ya kuialika Klabu ya Power Dynamos katika Tamasha la Simba Day huenda ikawa fursa kwa makocha wa timu zote mbili kusomana, na endapo timu hizo zitakutana tena katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa, basi makocha wote watakuwa na kumbukumbu nzuri ya kupambana ili kusaka nafasi ya kutinga hatua ya makundi.

Lakini pamoja na yote hayo, hii sio mara ya kwanza kwa Simba SC kuialika Power Dynamos katika Tamasha la Simba Day, kwani walifanya hivyo mwaka 2019.

Mchezo huo ambao ulipigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam ulishuhudia wenyeji Simba SC wakiibuka na ushindi wa mabao 3 -1.

Mabao ya Simba SC katika mchezo huo yalifungwa na Medie Kagere Kwenye (Hat trick) DK 3′, 58′ na 73′ huku bao la Power Dynamos likifungwa na Jimmy Dlingai DK 23′

Wakati Simba SC ikimsubiri mshindi wa mchezo wa mzunguuko wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kati ya Mabingwa wa Namibia African Stars dhidi ya Mabingwa wa Zambia Power Dynamos, upande wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans watacheza dhidi ya Mabingwa wa Djibout ASAS na kama watashinda watamsubiri mshindi wa mchezo kati ya Otoho D’Oyo ya DR Congo dhidi ya El Mereikh ya Sudan.

Mabingwa wa visiwani Zanzibar KMKM wao wataanzia nyumbani kwa kuikaribia St George ya Ethiopia kisha watakwenda kumalizia ugenini mjini Addis Ababa.

Mshindi wa mchezo huo atacheza na mshindi wa mchezo kati ya APR ya Rwanda dhidi ya Gaadidka ya Somalia.

Moises Caicedo ajisogeza Stamford Bridge
Wanaotoa Vitambulisho vya Taifa kwa wageni wasakwa