Boniface Gideon -Tanga.

Jumla ya Kaya 229 kutoka Vijiji mbalimbali Wilayani Mkinga Mkoani Tanga, zimepatiwa msaada wa Chakula kupitia Shirika la World Vision ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na uhaba wa Chakula kwenye baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na ukame kwa miaka miwili mfululizo.

Wakizungumza mara baada ya kukabidhiwa msaada huo, Wananchi wa Vijiji zaidi ya nane wilayani humo wamesema wamekuwa wakikabiliwa na uhaba wa Chakula kwa kipindi cha Miaka miwili sasa, jambo linalopelekea afya zao kudumaa na hatimaye watoto kushindwa kufanya vizuri shuleni.

“Watoto wetu wanatakiwa wale kutwa mara tatu lakini wakwetu kutwa wanakula mara moja tuu hii ni changamoto kubwa sana inayotukabili sisi wazazi tunanyongeka sanaa, tunasumbuliwa na Upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo katika Vijiji vyetu tunaiomba World Vision kuviwezesha na Vikundi vya Walemavu msaada wa Pembejeo,” wamesema.

Kwa Upande wake Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Duga Maforoni Wilayani Mkinga, Albertina Makungu amesema mwaka wa 2021/2022 walipatwa na changamoto ya ukame katika maeneo ya Wilaya ya Mkinga, na amelishukuru Shirika hilo kutoa msaada kwa watu wenye uhitataji.

Meneja wa Mradi wa World Vision Wilaya ya Mkinga, Evodia Chija amesema Shirika hilo kupitia Viongozi wao limeamua kuwagusa waathirika kutokana na ukame katika baadhi ya maeneo, ambapo wameweza kuwachangia Maharage na mahindi kilo 2000.

“Tumetoa msaada wa Maharage, unga kilo 2000 wenye virutubishi kwenye kaya hizi lakini kati ya kaya hizo Kaya 30 ni za watu wenye ulemavu, watoto ambao ni wasajiliwa kwenye miradi ya World Vision wako kaya 136,”alibainisha Chija.

Sakho amtaja Sadio Mane dili la Ufaransa
Dkt. Mwinyi ataka michango ZSSF iwasilishwe kwa wakati