Kocha wa Klabu ya Crystal Palace Roy Hodgson amesikitika kumpoteza Wilfried Zaha, aliyeihama klabu hiyo ya England na kujiunga na miamba ya Uturuki, Galatasaray.

Zaha, alikuwa mchezaji huru baada ya kumalizika kwa mkataba wake na Crystal Palace na alifichua kuwa alikuwa Istanbul kwa mazungumzo, baada ya kuripotiwa kukataa ofa ya mshahara wa Pauni 200,000 kwa juma ya kusalia pale Selhurst Park.

Mapema juma hili, alitumia Instagram kuthibitisha kuondoka kwake Palace, klabu ambayo alijiunga nayo akiwa na umri wa miaka 12 na kufunga mabao 90 katika mechi 458, akielezea jezi yao kama “ngozi yake ya pili”.

Baada ya Galatasaray kutangaza kuwa Zaha amesaini mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya pauni milioni 3.75 kwa mwaka, Hodgson alionesha kusikitishwa kwake na kuondoka kwa mshambuliaji huyo.

Hodgson alisema, “Nilihuzunika sana kusikia kwamba Wilf ameamua kuondoka na kuanza ukurasa mpya katika maisha yake ya soka. Siku zote nilikuwa na matumaini kwamba angeweka mustakabali wake kwa klabu na ningekuwa na manufaa ya kufanya naye kazi tena msimu huu.”

Kocha huyo amesema kuwa angependa kumshukuru yeye binafsi kwa yote aliyofanya wakati wake kama kocha.

“Klabu inapoteza mtu mashuhuri na, ingawa tunasikitika kwamba haikuwezekana kumshawishi Wilfried kukaa muda mrefu, tunaweza tu kumtakia kila la heri yeye na familia yake katika mradi wao mpya,” alisema kocha huyo.

Zaha aliondoka Palace na kujiunga na Manchester United mwaka 2013, lakini alirejea London kwa mkopo mara mbili kabla ya kurejea rasmi mwaka 2015.

Mchezaji huyo wa Kimataifa wa Ivory Coast, ambaye aliichezea England mara mbili kabla ya kubadili uraia wake, pia alikuwa akihusishwa na Lazio, Fenerbahce na Al-Nassr msimu huu wa majira ya joto.

Gavana Kortini kwa kumiliki Silaha kinyume cha sheria
Ruto, Odinga kuyajenga baada ya safari Tanzania