Uongozi wa Klabu ya Mtibwa Sugar upo kwenye mazungumzo ya kumpata aliyekuwa mshambuliaji wa Ruvu Shooting, Abalkassim Suleiman ili akaitumikie timu yao kwa msimu ujao, huku ikielezwa ni pendekezo la Kocha Mkuu wa timu hiyo, Habibu Kondo.

Afisa Mtendaji mkuu wa timu hiyo, Swabri Aboubakar amesema wachezaji wote waliopendekezwa na benchi la ufundi tayari wameanza nao mazungumzo ya kuwaongeza katika kikosini chao.

“Tumeondokewa na wachezaji wengi ila siyo sababu ya sisi pia kushindwa kusajili wengine, tunaamini usajili wetu wote utakapokamilisha basi mashabiki wetu watafurahi kwa sababu hiyo ndio kiu yetu kubwa,” amesema.

Kwa upande wa Abalkassim amesema kwa sasa bado ni mapema kuzungumzia hilo kwa sababu zipo timu nyingi ambazo zimeonyesha nia ya kuhitaji saini yake, na bado hajaamua kufanya maamuzi ya mwisho ya wapi atacheza msimu ujao.

Awali Abalkassim alihitajika na klabu ya West Armenia lakini walishindwana kwenye suala la maslahi binafsi.

Nyota huyo aliyefunga mabao manne na Ruvu Shooting iliyoshuka daraja ataungana na mastaa kama Kelvin Nashon na Yassin Mustapha waliotokea Singida Fountain Gate na Matheo Anthony aliyeachana na KMC.

Dodoma Jiji FC yaweka ramani mezani mapema
Miili 901 imepatikana pwani - Waziri Mambo ya Ndani