Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani – WHO nchini, Dkt. Charles Sagoe-Moses ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kufanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Afya pamoja na kutoa ushirikiano kwa mashirika ya Kimataifa ikiwemo WHO.

Dkt. Sagoe-Moses ametoa pongezi hizo hii leo Julai 28, 2023 wakati akiwasilisha hati za Utambulisho kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax katika Ofisi Ndogo za Wizara zilizopo jijini Dar es Salaam.

“Ninaipongeza Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wenu ambao mmekuwa mkiutoa kwa Shirika la Afya Duniani, hakika tunaahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano katika kuhakikisha kuwa tunaboresha na kuimarisha misingi ya sekta ya afya hapa Tanzania,” amesema Dkt. Sagoe-Moses.

Ameongeza kuwa, juhudi za Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na magonjwa ya mbalimbali hasa yale ya mlipuko zinaridhisha, na kutolea mfano jinsi Tanzania ilivyopambana na homa ya Marburg katika mkoa wa Kagera.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax amesema Tanzania itaendelea kufanya kazi na WHO ili kuhakikisha inaboresha na kuimarisha mifumo ya afya na Sekta ya afya na utekelezaji wa afua mbalimbali za mapambano dhidi ya magonjwa.

Tanzania, imekuwa ikishirikiana na WHO pamoja na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi, kuhakikisha inaboresha mifumo ya afya na Sekta ya afya, ili kuijengea uwezo nchi na wataalam wake katika kutambua na kudhibiti magonjwa.

GGML yatoa msaada wa madawati 8,823 Geita
NiRC kuja na mageuzi utekelezaji sekta ya umwagiliaji