Eva Godwin – Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma – DUWASA, Mhandisi Aron Joseph amesema ukosefu wa Maji katika Chuo Kikuu cha Dodoma na jiji kiujumla ni aibu na kwamba Wananchi wakilalamika kuhusu upatikanaji wa hitaji hilo, ni kuikosea Tanzania.

Mhandisi Aaron ameyasema hayo hii leo Julai 28, 2023 wakati akizungumza na Waandishi wa habari leo Jijini Dodoma juu ya utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka na mwelekeo wake kwa mwaka 2023-2024 na kudai kuwa wamejipanga kuhakikisha wanaimaliza kero hiyo.

Amesema, “jiji kubwa kama hili kukosa maji ni aibu kubwa sana, tutachimba visima 1845 na chuo kikubwa kama kile hakitakiwi kutoa Maji lita 60 kwahiyo tutatoa kuanzia lita 70 na kuendelea juu, ili upatikanaji wa Maji uwe rahisi.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma – DUWASA, Mhandisi Aron Joseph.

Aidha, Mhandisi Aron amesema, “Nchi yote ipo Dodoma kwaio tukisikia Wananchi wanalalamika kuhusu upatikanaji wa Maji tutakuwa tunaikosea Tanzania kwa ujumla , hivyo tuwahakikishie tu mradi huu wa uchimbaji wa visima unaoenda kuanza utapunguza ukosefu wa Maji kuanzia Mjini na Vijijini.”

Hata hivyo, Aron amesema chanzo kikuu cha maji kwa matumizi ya wakazi wa mji wa Dodoma ni visima virefu vilivyochimbwa katika bonde la Makutupora eneo la Mzakwe na kwamba miundombinu ya uzalishaji maji pamoja na uwezo wa usafirishaji maji ni lita milioni 61.5 kwa siku.

Amevitaja vyanzo vingine vidogo vya maji kwa maeneo mahsusi ambayo ni Ihumwa kwa ajili ya Mji wa Serikali, Iyumbu kwa ajili ya Chuo Kikuu cha Dodoma , Kata ya Iyumbu, Hospitali ya Benjamini Mkapa na Kata ya Ng’hong’onha, ambavyo kwa pamoja vinazalisha lita 5.6 milioni kwa siku.

“Hivyo upungufu wa maji katika mji wa Dodoma ni lita milioni 64.8 kwa siku. Upungufu huu unaongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na ongezeko la watu na shughuli za kiuchumi na kijamii mjini Dodoma”. Amebainisha Muhandisi Aron.

Malimwengu: Aachiwa huru kwa kesi ya Wafungwa 26
GGML yatoa msaada wa madawati 8,823 Geita