Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Zambia na Klabu ya Simba SC Clatous Chota Chama, amesema kurudi kwa Luis Miquissone klabuni hapo, ni ishara ya kikosi chao kurejea katika makali ambayo walikuwa nayo misimu mitatu iliyopita.
Miquissone amerejea Simba SC baada ya kuondoka tangu mwaka 2021 ambapo aliuzwa kwa Mabingwa wa Soka Barani Afrika Al Ahly ya Misri kabla ya kuvunja mkataba hivi karibuni.
Akizungumza mjini Ankara-Uturuki ambako Simba SC imeweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya, Chama amesema alikuwa anawasiliana na Miquissone alipokuwa Misri, alihitaji kurudi Simba SC kwa muda mrefu.
Chama amesema alifurahi alipoona mchezaji huyo, ameanza utaratibu wa kurudi Simba SC na alikuwa akiongea naye mara kwa mara.
“Luis alikuwa anatamani sana kurudi Simba SC kuja kuendeleza kipaji chake, hivyo siyo vizuri kwa mchezaji kufanya kazi na watu ambao hawakupi furaha ya moyo hata kama unalipwa fedha nyingi.
“Mimi naamini kuwa msimu ujao tutafanya vizuri sana, naomba Mungu aendelee kutujalia uzima na afya, mimi na Luis na wachezaji wenzangu, hivyo ninaamini mashabikí kwa ujumla watafurahi.
Miquissone, amepewa mkataba wa miaka miwili ambapo atalipwa mshahara wa zaidi ya sh. milioni 30 kwa mwezi.
Kutua kwa Miquissone, kunaifanya Simba SC iongeze nguvu eneo la mbele ambalo tayari lina maingizo mapya, Aubin Kramo kutoka ASEC Mimosas ya Ivory Coast, Willy Onana aliyekuwa Rayon Sports ya Rwanda, Shaaban Chilunda kutoka Azam FC na Fabrice Ngoma aliyekuwa timu ya Al Hilal ya Sudan.
Mbali na hao, kikosini wapo Kibu Denis, Peter Banda, Moses Phiri, John Bocco na Saido Ntibazonkiza.