Siku tatu zikisalia kabla ya kikosi cha Simba SC kuanza safari ya kurejea Tanzania kutoka Uturuki, Kocha Mkuu wa klabu hiyo Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema ameridhishwa na utimamu wa mwili walionao wachezaji wake kwa sasa na hiyo itawasaidia kuepuka majeraha madogo madogo.

Roberthino, amesema siku tatu zilizobakia atazitumia kuongeza makali kwenye safu yake ya ushambuliaji ambayo msimu ujao itakuwa chini ya Luis Miquissone, Aubin Kramo, Willy Onana, Jean Baleke, Denis Kibu, Iddi Chilunda, Moses Phiri na nahodha John Bocco.

Akizungumza mjini Ankara-Uturuki, Robertinho amesema ameona wachezaji wake wengi wakiwa na utimilifu wa mwili na hii inampa matumaini ya kuwa na kikosi imara.

“Hii ni muhimu kwa sababu huko mbele hawatoweza kupata tena nafasi ya kuwajenga sana zaidi ya kuwarudishia tu ufiti unaopotea kwa sababu tutakuwa na mashindano mengi, nalipongeza benchi langu la ufundi upande wa mazoezi ya viungo, angalia kwa sasa sisikii habari ya wachezaji wenye matatizo ya misuli na hiki ni kitu kizuri sana na kitatusaidia mbele ya safari,” amesema kocha huyo raia wa Brazil na kuongeza,

“Nimeridhika na kikosi changu pamoja na maandalizi yote tunayofanya kambini, nikwambie tu kwa sasa tuna vikosi viwili vyenye uwezo unaofanana,” amesema kocha huyo huku akitoa pongezi kwa wasaidizi wake wa mazoezi ya viungo.

Jopo la makocha wa viungo la timu hiyo msimu huu linaongozwa na Corneille Hategekimana raia wa Rwanda.

Robertinho amesema kwa sasa anakamilisha Program yake aliyokuwa ameiandaa kwa ajili ya kambi ya nchini húmo na watarejea nchini wakiwa na kikosi imara.

Simba SC inatarajia kurejea nchini Agosti Mosi tayari kwa tamasha lake la ‘Simba Day’ ambalo kilele chake kitakuwa Agosti 6.

Simba SC itacheza mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki siku hiyo ya kilele cha Simba Day na baada ya hapo inatarajia kuelekea jijini Tanga kwa ajili ya michezo ya Ngao ya Jamii.

Kikosi hicho cha Robertinho kitacheza na Singida Fountain Gate na mshindi wa mechi hiyo atacheza na mshindi wa mechi kati ya Young Africans na Azam FC kupata timu mbili zitakazocheza mchezo wa mwisho kuwania Ngao ya Jamii kwa msimu mpya wa 2023/2024.

David Silva akubali yaishe
Ndunguru akemea lugha chafu, kejeli kwa wagonjwa