Kocha Mkuu wa Manchester City Pep Guardiola, ameionya Ligi Kuu England kwamba fedha zinazotolewa nchini Saudi Arabia zimebadilisha soko baada ya kumpoteza winga, Riyad Mahrez kwenda Al Ahli.

Mahrez ni mmoja wa nyota wakubwa ambao wamemfuata Cristiano Ronaldo Mashariki ya Kati msimu huu wa majira ya joto.

Akiwa hakutarajia kumpoteza Mahrez msimu huu wa majira ya joto, Guardiola amesisitiza kuwa City haitatafuta mbadala wa moja kwa moja wa Mualgeria huyo, lakini akakiri kwamba Mshambuliaji wa aina yake hawezi kufika Etihad.

“Hatutafuti mbadala wa Riyad katika suala la ustadi kwa sababu kila mchezaji ni tofauti,” amesema Guardiola.

“Tutaona kitakachotokea kwa wachezaji wa mkopo na ni wachezaji gani watakaa hapa. Mambo machache yatafanyika.”

Guardiola ameendelea kuwaonya wachezaji wengine wa Ligi Kuu England kwamba matumizi ya fedha kwenye Ligi Kuu ya Saudia yamebadilisha sana soko la uhamisho na kuziacha hata timu kubwa za England zikishindwa kushikilia vipaji vyao vya juu.

“Saudi Arabia imebadilisha soko,” ameeleza.

“Miezi michache iliyopita, wakati Cristiano ndiye pekee aliyeondoka, hakuna aliyefikiria kuwa wachezaji wengi wa juu zaidi wangecheza kwenye Ligi ya Saudia.

“Katika siku zijazo kutakuwa na zaidi na ndiyo maana klabu zinahitaji kufahamu kinachoendelea. Riyad alipata ofa ya ajabu na ndiyo maana hatukuweza kusema ‘usifanye’.”

City, wakiwa wamempoteza pia nahodha Ilkay Gundogan aliyejiunga FC Barcelona msimu huu wa majira ya joto, wanamenyana na Bayern Munich ili kumbakisha beki wa kulia Kyle Walker, ambaye amepokea ofa kutoka kwa mabingwa hao wa Bundesliga.

Mrithi wa Mayele atoa kauli ya kibabe
Rais ZFF: Dhamira yangu ina maono ya mbali