Baada ya kumaliza kambi ya Majuma matano nchini Tunisia, Azam FC imetamba kuanza msimu wa mwaka 2023/24 kwa Kutwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii.

Akizungumza jijini Dar es salaam Afisa Habari wa Azam, Hashim Ibwe amesema kuwa msimu huu hawataki mchezo, kwani dhamira yao ni kuhakikisha wanasepa na mataji yote ya ndani na kufika mbali kwenye michuano ya Kimataifa.

Amesema kuwa kwa kuanzia wataanza kutwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii na mengine kufuatia, kwani wamesajili na kujiandaa vizuri na wako tayari kufukuzia mataji.

Timu hiyo iliyopanda Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 2008, hawajawahi kutwaa Ngao ya Jamii na kama wakiitwaa itakuwa mara yao ya kwanza, huku wakitwaa taji la Ligi Kuu mara moja tu msimu wa 2013/14.

Karata yao ya kwanza itakuwa dhidi ya Young Africans mchezo unaotarajiwa kuchezwa Agosti 9, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.

Ibwe amesema wamemaliza kambi yao salama ambayo waliiweka katika mazingira magumu na Kocha Mkuu Youssoupha Dabo amepata alichokitaka kwenye maandalizi yake na sasa wako tayari kwa ajili ya mashindano.

“Kazi nzuri imefanyika kwa benchi la ufundi kilichobaki sasa ni kazi kwa wachezaji kukifanyia kazi kile walichokipata kutoka kwa makocha wao,” amesema Ibwe.

Aidha, Ibwe amesema wameandaa gari kwa ajili ya mashabiki wao wanaotaka kwenda kuipa sapoti timu jijini Tanga na safari hii wamepanga kwenda kuwafurahisha sio kuwavunja moyo na dhamira yao taji lao la kwanza msimu huu ni Ngao ya Jamii.

Katika hatua nyingine, Ibwe amesema kuwa hali ya beki Charles Manyama inaendelea vizuri, na kwa sasa anafanya mazoezi mepesi ili aweze kukaa sawa kabla ya kurudi kuipambania timu.

Ujuzi wa kutosha: Walimu wajengewe uwezo - Soraga
Mtaji UTT AMIS wafikia Trilioni 1.5