Shirikisho la Soka Afrika ‘CAF’ limetajwa kuchelewesha ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2023/24, kufuatia kutambulishwa kwa Michuano ya African Football League (Super Cup), ambayo itachezwa kwa mara ya kwanza mwaka huu 2023.

Tayari ya Bodi ya Ligi Tanzania Bara ‘TPLB’, imeeleza kuwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2023/24, itaanza rasmi Agosti 15, mwaka huu, lakini bado haijatangaza ratiba ya ligi hiyo.

Akizungumza jijini Dar es salaam Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania Bara ‘TPLB’ Almasi Kasongo, amesema ratiba kwa mashindano yote ambayo yalikuwa tangu hapo nyuma kila kitu kimekaa vizuri, yakiwamo Mapinduzi Cup, kuwania kufuzu CHAN na mengineyo.

“Nina uhakika kabisa mpaka itakapofika wiki ijayo, tutakuwa tumekamilisha hilo zoezi na kuweza kutangaza ratiba yetu ya msimu wa 2023/24,” amesema Kasongo.

“Kama unavyojua ratiba ya Ligi Kuu inaakisi na mshindano mengine, kama Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho ambalo tayari CAF wameshatoa ratiba yake, lakini sasa imeongezeka African Super Cup na moja ya timu shiriki ni Klabu ya Simba SC,” amesema Kasongo na kuongeza:

“Mpaka sasa Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, halijatoa ratiba zaidi imetaja tu tarehe ya ufunguzi wa mashindano hayo na mechi itachezwa wapi, lakini kwa maana ya ratiba nzima bado hawajaitangaza na unaona jinsi wanavyokwamisha zoezi zima la ratiba yetu kuweza kuakisi ratiba ya mashindano hayo.

“Hatujui hata mashindano hayo yanachezwaje, imetaja tu itafanyika kati ya mwezi wa 10 na 11, hivyo inachezwaje bado ni kitendawili.”

Lushoto hawajakata tamaa, wana jambo lao
Eriksen: Hojlund ni balaa kabisa