Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amewaondoa presha mashabiki wa timu hiyo kwa kuwaambia muda walioupata katika kambi yao nchini Uturuki, umewasaidia kuwajenga vizuri wachezaji wa timu huyo kwa ajili ya msimu ujao 2023/24, huku akiamini kazi ya ubingwa kwao haitokuwa ngumu.
Robertinho ametoa kauli hiyo baada ya Simba SC kukamilisha kambi yake nchini Uturuki tayari kwa kuanza msimu wa 2023/24.
Akizungumza baada ya kuwasili jijini Dar es salaam mapema leo Jumatano (Agosti 02) majira ya alfajiri, Kocha Robertinho amesema licha ya kupata muda wa majuma matatu ambayo ni chache kwenye kujenga timu, lakini ameweka sawa kila kitu akishirikiana na wataalamu wengine kwenye benchi la ufundi.
Amesema wasaidizi wake walifanikiwa kumsaidia katika mbinu za kiufundi kwa wachezaji kuelewa haraka kile alichowapa kwenye mazoezi na kuamini kambi hiyo imeleta mapinduzi makubwa.
“Tumefanya kazi mambo mengi katika kipindi hiki, ikiwemo utimamu wa miili, umoja, ushirikiano, mbinu na mifumo tutakayoitumia mara kwa mara katika mechi zetu za ndani na kimataifa, kwa wachezaji kuonekana kuelewa kwa haraka zaidi.
“Nataka kila kitu kimalizike katika muda muafaka ili kuwa tayari kwa msimu mpya, michezo ambayo tumecheza tukiwa kambini kwa namna kubwa imeweza kutujenga kiasi fulani, uwezo wa wachezaji wapya umeendelea kuimarika, nadhani mashabiki wapunguze presha matumaini yetu ni makubwa sana,” amesema Robertinho.