Serikali imewatoa hofu watanzania na kusema inaendelea na mchakato wa kumpata mkandarasi wa kuanza ujenzi wa Uwanja wa kimataifa mkoani Dodoma.

Pamoja na uwanja wa Dodoma, imesema ipo katika mchakato wa kujenga viwanja mbalimbali vya wazi na kukamilika ndani ya miezi 24.

Akizungumza jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Ally Mayay, amesema adhma ya serikali ya kujenga uwanja wa mpira wa kimatafa Dodoma ipo palepale.

“Serikali inaendelea kukamilisha utaratibu wa kumpata mkandarasi ujenzi utaanza mara moja, watanzania wasiwe na hofu” amesema.

Kuhusu ujenzi wa viwanja vya wazi, Mayay amesema mkandarasi yupo kazini na shughuli za ujenzi zinaendelea.

Amevitaja viwanja vya wazi vitakavyojengwa kuwa ni vya netiboli, kikapu, mpira wa mikono na mpira wa wavu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi wa Mkoa wa Dodoma, wameiomba Serikali kuharakisha ujenzi wa viwanja hivyo lengo likiwa kuongeza mwamko wa watu kupenda michezo.

Mkazi wa Kata ya Chamwino, Samson Chisili, amesema Dodoma ni makao makuu ya nchi hivyo lazima iwe na uwanja wa kisasa.

Chisili amesema Serikali inapaswa kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa mkandarasi na kuanza ujenzi huo mara moja kwani umepita muda mrefu tangu ilipotangaza kujenga uwanja huo.

Pili Shaban amesema atafurahi kuona mashindano mbalimbali ya kimataifa yanafanyika katika uwanja wa Dodoma hivyo ujenzi wake usichelewe.

Virgil van Dijk kuvaa kitambaa Liverpool
GGML kushirikiana na TANESCO umeme gridi ya Taifa