Mbunge wa Kigamboni, Dkt. Faustine Ndugulile ametaka Asasi za Kiraia – AZAKI, kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia mabadiliko ya kiteknolojia na hali ya kisiasa ilivyo ambayo inaweza athiri kazi zake kutokana na kupungua kwa ufadhili na uwepo wa mifumo ya kisera isiyo rafiki.
Dkt. Ndugulile ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa wiki ya AZAKI jijini Dar es Salaam na kudai kuwa hata hivyo uchumi wa Viwanda, watu, sera na utekelezaji wa wiki hiyo umekuwa ni jukwa kubwa la majadiliano linaloongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu ya kila siku kiutendaji.
Amesema, “Hali ya Kisiasa imebadilika na maradhi ya Uviko-19 pia yaliathiri ulimwengu mzima hali hii inaweza athiri CSO kwa wafadhili kuona pesa zao ni za kwao kwanza na ufadhili unapungua maana Wabunge wa Mabunge ya nchi watoa misaada, baadhi yao hawaungi mkono utoaji wa fedha za ufadhili.”
Aidha, Ndugulile ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia na Mgeni Maalum katika ufunguzi huo wa wiki ya AZAKI, pia amesema misaada kwasasa imekuwa ya nipe nikupe na kwamba hutolewa kwa masharti na imekaa kimfumo faida tofauti na ilivyokuwa hapo awali hivyo AZAKI ziendeshwe kwa kuzingatia mahitaji ya sasa.