Nguli wa Utangazaji nchini Tanzania, Hamza Kassongo ameimwagia sifa Dar24 Media baada ya kufanikiwa kutwaa tuzo saba za umahiri katika Uandishi wa Habari – EJAT, kwa msimu wa mwaka 2022/23.

Kassongo ametoa pongezi hizo wakati alipokuwa akizungumza na Meneja wa Dar24 Media, Abel Kilumbu aliyemtembelea nyumbani kwake Masaki, jijini Dar es Salaam na kusema kushinda tuzo saba za EJAT ni jambo kubwa linalotoa tafsiri ya ubora wa kituo hiki katika maudhui yake.

Meneja wa Dar24 Media, Abel Kilumbu (kushoto), akifurahia jambo na Nguli wa Utangazaji nchini Tanzania, Hamza Kassongo alipomtembelea nyumbani kwake Masaki, jijini Dar es Salaam.

Amesema, “si rahisi kushinda tuzo EJAT, lakini ninyi mmeweza kushinda tena kwa rekodi kubwa kuliko vyombo vingine vya habari,. Nawapongeza sana na kupitia hili naona mabadiliko makubwa sasa jinsi watu wanavyoanza kuchukulia kwa umuhimu mkubwa zaidi vyombo vya habari vinavyorusha maudhui yake kwa njia ya mitandao ya kijamii.”

Hamza Kassongo akiitazama Fulana yenye Nembo ya Dar24 Media, aliyokabidhiwa na Meneja, Abel Kilumbu.

Nguli huyo pia ameitaka Dar24 media kujikita zaidi kwenye habari za uchunguzi pamoja na tafiti, huku akitoa rai kwa uongozi wa DataVision International unaoisimamia Dar24 Media kuanzisha kituo cha Redio Dar24, ili kuwafikia watu wengi zaidi.

Hamza Kassongo ni Mwanahabari Mwandamizi aliyetunukiwa tuzo ya maisha ya umahiri katika Uandishi wa Habari mwaka 2013, na tangu astaafu kazi ya utangazaji, ni Dar24 media pekee ndiyo iliyofanikiwa kuwahi kufanya naye mahojiano maalumu.

Pongezi hizo, zinatolewa ikiwa ni kipindi kifupi tangu Dar24 Media ilipoweka rekodi kwenye tuzo za EJAT, baada ya kufanikiwa kunyakua tuzo saba kupitia Waandishi na Watangazaji wake mahiri saba, waliongia kwenye tuzo hizo kubwa zaidi za Uandishi wa Habari nchini Tanzania.

Polisi yathibitisha vifo vya wanne Familia moja Chalinze
Tunawatambua Wahandisi ukuzaji wa uchumi - Dkt. Mwinyi