Kocha Mkuu wa Simba SC, Robert Oliveira ‘Robertinho’ amesema anahitaji muda zaidi kuweza kuiunganisha timu hiyo icheze vile anavyotaka na kupata matokeo mazuri zaidi.
Simba SC juzi Jumapili (Agosti 06) iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Power Dynamos ya Zambia kwenye mchezo wa kirafiki wa kilele cha tamasha la klabu hiyo maarufu kama Simba Day Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mabao ya Simba SC kwenye mchezo huo yalifungwa na nyota wao wapya Willy Onana aliyefunga kipindi cha kwanza na lingine likifungwa na kiungo Fabrice Ngoma kipindi cha pili.
Roberinho amesema kuwa amefurahishwa na ushindi huo ingawa anahitaji muda zaidi kuweza kukiunganisha kikosi cha timu hiyo kucheza kitimu zaidi na kumpatia matokeo.
“Ni matokeo muhimu kwa timu yangu kwani baada ya kambi ya Uturuki tulihitaji kupata ushindi kujenga hali ya kujiamini zaidi. Lakini bado nahitaji muda zaidi kuweza kuwaunganisha wachezaji wangu wacheze kitimu,” amesema Robertinho.
Amesema kambi ya timu hiyo nchini Uturuki ilikuwa na msaada mkubwa kwani walipata utulivu wa kutosha wa kuwaelekeza wachezaji namna gani wanataka wacheze na kuiletea timu hiyo mafanikio kwenye mashindano yote yaliyo mbele yao.
Tuna mashindano muhimu kama vile Ngao ya Jamii, Ligi na Supa Ligi ambayo maandalizi yake yanaenda pamoja. Tayari nina kikosi cha kwanza ingawa naendelea kuangalia zaidi na zaidi wachezaji wengine kupata kikosi kipana,” amesema Robertinho.